Wednesday, October 6, 2010

FURAHA KATIKA MAHUSIANO NA NDOA


Leo ukiangalia ndoa nyingi zimepooza na kufunikwa na wingu zito la mizozo kila kukicha,ukiwauliza wanandoa wengi husema Mwanzoni mwa ndoa yetu tulipendana kwa dhati,lakini shauku na penzi letu siku hizi imepotea,hakuna urafiki mzuri kati yetu kama hapo awali wala hatufurahii kuwa pamoja,hata kucheka inakuwa tatizo pamoja na kulala kitanda kimoja na ushirika wao katika mambo mengi, lakini mambo yanakuwa hayaendi,ndoa zingine wana ndoa hawawezi hata kujadili matatizo yao kwa pamoja,,mbaya zaidi kufanya mapenzi kwao imekuwa kama wajibu badala ya starehe,hii ni hatari maana hakuna mtu kati yao anayejisikia shauku ya mapenzi kwa mwenzi wake,ukichunguza sio kwamba kuna mtu anatoka nje ya ndoa hapana utawasikia wanasema ndoa yetu haina upendo.Matatizo ya ndoa yapo mengi na yanatofautiana ndoa na ndoa,lakini vilio vingi vya ndoa vinafanana,swali kubwa hapa ni kutaka kujua ni jinsi gani unaweza kuifurahia ndoa yako pamoja na changamoto nyingi unazokutananazo kila kukicha.Hebu tuangalie baadhi ya mambo yanayoweza kuifikisha ndoa yako kwenye furaha isiyo kifani na ya kusisimua.

                                                       
                                                  Jambo la kwanza
                                                      1: UPENDO

Tatizo la watu wengi ni kwamba hawajui nini maana ya upendo, na wengi wanafikiri wanafahamu lakini ukiangalia kwa undani utagundua kuwa kile wanacho kijua na kukiamini kuhusu upendo hakina  ukweli wowote. Leo ukizunguka kila mahali utakutana na watu wengi wamechanganyikiwa kwa kutojua maana ya upendo. hili si tatizo la mtu mmoja au wawili bali ni tatizo ambalo limetapakaa dunia nzima. Ajabu ni kwamba unaweza kukuta watu wanazungumza juu ya upendo lakini kwa makini ukichunguza utaona hawajui maana yake. Leo matatizo mengi katika ndoa yanasababishwa na kutopendana kati ya mume na mke hii ni pamoja na kutojua nini maana ya upendo au penzi.
Upendo ni nini? Upendo ni vitendo vya ukarimu, ni tendo tufanyalo, sio kujisikia, ni kufanya vitendo vya ukarimu na kuzungumza maneno ya upole na fadhili, upendo ni kutoa na kusameheana, ni kusaidiana, ni shukurani, ni tabasamu, ni kupongeza na vitendo vingine vingi vinavyofanana na hivi. Hapa ndio linakuja tatizo la watu wengi ambao huamini kuwa upendo ni kitu ambacho kinaweza kupotea au kutoweka. Unajua ni rahisi kusimama na kusema kuwa “Upendo au penzi letu kwenye ndoa yetu limepotea” Hapa ukweli halisi ni kwamba upendo hauwezi kupotea kwa sababu upendo au penzi ni vitendo, hivyo unaweza kuchangua kutenda vitendo vya upendo au usichague kufanya hivyo. kama utachagua kuwa mwenye huruma, kusaidia, kusema kweli hapoutakuwa umechagua kupenda, lakini bado unaweza ukachagua kutokupenda pia. Unaweza kuchagua kutokuwa na subira wala msamaha na ukachagua kutompenda mwenzi wako, hapo hauwezi kusema kuwa pendo au penzi lako limepotea. Hivyo ni vizuri mtu akatambua kuwa upendo ni kuchagua kufanya vitendo vya ukarimu.
                                                              Jambo la pili
                                                      2: HISIA ZA MAPENZI



Hisia ya penzi ni nini? Hisia ya penzi ni ile hali isiyo kifani, msisimko moyoni, na kujisikia mchangamfu na mwenye raha umwonapo mpenzi wako. Ni hisia nzuri kwa kweli kuwanayo, ni nzuri kupindukia ndiyo maana hata nyimbo na mashairi yameandikwa juu yake. Wengi wetu tumekwisha patwa na hisia hizi, Pengine ulikuwa kijana mdogo sana wakati unapatwa na hisia za mapenzi kwa mara ya kwanza. Mapigo yako yalikwenda mbio mara mia zaidi kila mara anapokutazama, na baadaye mlipoahidi kuoana  na huyo ambaye hivi sasa ni mkeo au mumeo, pengine hisia zako kwa wakati huo zilikuwa na nguvu sana. Hata hivyo kuna ukweli mmoja kuhusu hisia za mapenzi ambao ni watu wachache tu wanao ufahamu, kwamba hisia za mapenzi huja na kutoweka, leo mtu anaweza kuwa na hisia za mapenzi lakini kesho zikatoweka, na baadaye kidogo zikarejea tena na pengine baada ya mda kidogo zikatoweka tena, na baadaye zikajitokeza tena, kwa nini? Kwa sababu hisia za mapenzi ni hisia tu na hisia zetu daima hubadilika. Sisi binadamu tuna hisia za aina nyingi, mara nyingine hujisikia mwenye huzuni na majonzi, lakini siku nyingine hujisikia mwenye furaha, wakati mwingine hujisikia umejawa na msisimko wa furaha, wakati mwingine hujisikia mwenye hasira na wakati mwingine hujisikia mpweke, vile vile wakati huja tunajikuta tunajisikia kupenda,  lakini hatukai na hisia hiyo hiyo kila siku, hii ni kwa sababu hisia zetu zinabadilika, sijui kama kuna mtu ambaye ameshawahi kuwa mwenye furaha kila siku mwaka mzima, hili haliwezekani maana furaha ni hisia tu hivyo huja na kutoweka, ni muhimu sana kila mtu kutambua kuwa  hisia zetu huja na kisha zinatoweka, na hii ni pamoja na hisia za mapenzi. Katika ndoa za kikristo bwana bibi arusi huahidi kupendana hadi watakapokufa, swali hapa, ni je kusema hivyo wanamaanisha kuwa wameahidi kuwa na hisia za mapenzi kila siku hadi kufa? Hapana, wanapo ahidi kupenda, wanakuwa wameahidi kufanyiana vitendo vya upendo kati yao kwa kipindi chote cha uhai wao, wana ahidi kuendelea kuwa wakarimu, kusaidiana, kuelewana, kusikilizana vile vile kusameheana na matendo mengine mengi ya kufanana na haya. Je, unaweza kuwa na hisia za penzi? Ndiyo, lakini sio kwa wakati wote, siku nyingine unaweza ukawa na msisimko mkali na hisia motomoto za mapenzi, lakini wakati mwingine unaweza ukawa na hisia tofauti, unaweza kujisikia mwenye hofu moyoni au pengine kuvujika moyo au kukasirika na hivyo kutokuwa kabisa na hisia za mapenzi moyoni mwako, hali ya namna hii inapokutokea usiogope maana ni hali ya kawaida kabisa kutokea. Mungu hajatuamuru tuwe na hisia Fulani tu, bali ametuamuru kupenda. Kwa hiyo mume na mke lazima wa waendelee kupendana kwa vitendo, hisia zitakuja na kutoweka wala hakuna haja ya kuwa na wasiwasi juu ya hilo maana ni jambo la kitambo kidogo tu, jukumu kubwa katika ndoa ni  kupendana tu kwa maneno ya upole na kwa vitendo na kuendelea kufanya hivyo kila siku. Lazima ujue hili kuwa hatuwezi kudhibiti hisia zetu bali tunaweza kudhibiti vitendo vyetu, hatuwezi kuchagua kuwa na hisia za fulani lakini tunaweza kuchagua kufanya vitendo vya aina fulani. Kwa mfano unaweza kushawishika kumkaripia mwenzi wako, lakini badala yake ukachagua kuongea naye kwa maneno ya upole, hapo utakuwa umechagua kumpenda mwenzi wako, hata kama unajisikia kuwa mchoyo na kutaka kujipendelea, unaweza bado ukachagua kumjali mwenzi wako, unaweza kumsikiliza na kujaribu kumwelewa kila anapozungumzia matatizo yake,, unaweza kuchangua kumfariji na kumtendea matendo ya upendo hata kama hisia zako zinakushawishi uwe mchoyo na mbinafsi. Kuna wakati unaweza ukajisikia kumhudumia mwenzi wako lakini pia kuna wakati unajisilia kujifurahisha mwenyewe, katika hali kama hii unachopaswa kujua ni kuwa upendo ni kumhudumia na kumjali mwenzi wako hata kama haujisikii kufanya hivyo. Unapochagua kumhudumia mwenzi wako unaweza ukawa haufuati hisia za wakati huo lakini ukawa unatimiza ahadi uliyo ahidi siku ya arusi yenu, tunaahidi kuwapenda wenzi wetu kwa sababu tunaweza kuchagua vitendo vyetu na sababu nyingine ni kwamba upendo hauko nje ya udhibiti wetu, tunaweza kupenda tukitaka.
Ufanye nini hisia za mapenzi zinapotoweka kabisa?


Hata kwenye ndoa imara hisia za mapenzi huja na kutoweka, hisia za mapenzi zinapotoweka mtajikuta hamjisikii kupendana kabisa na hali yenu kwenye ndoa yenu inakuwa mbaya sana, hili ni tatizo kubwa kabisa maana linaiweka ndoa kwenye hatari na muyumbo mkubwa sana. Ndoa yako ikifikia hatua kama hii basi kumbuka mambo yafuatayo.
Ø  Hata kama hisia zako zimetoweka: mpende mwenzi wako wa ndoa, mpende kwa vitendo vya ukarimu na uwe mwangalifu kumsaidia, uwe mpole, mkarimu, mwaminifu na mwenye kujitoa.
Ø  Kadri unavyoendelea na vitendo vya upendo ghafula utaanza kuona hisia zako za mapenzi zinarejea, huu ni ukweli kwamba hakuna haja ya kuishi pamoja katika ndoa bila hisia za mapenzi kati yenu. Hisia zenu zama penzi zitarudi iwapo tu mtaendelea kutendeana vitendo vya upendo. Hakika hisia za ampenzi ni hisia tu, hauwezi kuwanazo kila siku, zitakuja na kutoweka lakini haupaswi kuwa na wasiwasi. Kama utachagua kupenda kwa vitendo ni dhahili kuwa hisia zako za penzi haziwezi kupotea kwa mda mrefu.
Mkiacha kufanyiana vitendo vya upendo matokeo yake ni kutoweka kabisa kwa hisia zenu za mapenzi. Wanandoa wengi mda mfupi baada ya ndoa yao wanakuwa wapole na wakarimu kati yao lakini baada ya mda mfupi wanashindwa kuwa makini na wanaacha kutendeana vitendo vya upendo, badala yake wanaanza kukosoana, kukashifia, na kutoaminiana, vitendo kama hivi kwa hakika huondosha hisia za mapenzi mioyoni mwa wanandoa. Lakini mkiamua kutendeana vitendo vya upendo,msisimko wa hisia za mapenzi utarudi. Hebu tuseme wewe leo una hisia nzuri ajabu kwa mke wako mpenzi, kwa hakika ni mwanamke mzuri na wakupendeza ajabu. Lakini huyo mkeo amefanya jambo Fulani linalokuudhi sana, kadri unavyofikiria jinsi mkeo alivyokuudhi ndivyo na hisia zako za mapenzi moyoni mwako zinabadilika taratibu na kuwa hisia za hasira na chuki. Ndipo unakuja uchaguzi, kama unataka unaweza kuchagua kutokuwa na subira au msamaha kwa mkeo kwa maneno mengine ni kwamba unaweza kuchagua kutompenda mkeo, au kama ukitaka unaweza kuchagua kumfahamisha kwa njia ya upole na kumweleza jinsi alivyokuudhi na baada ya hapo ukamsamehe na kusahau, ni chaguo lako unaweza kupenda kama unataka .
Betty alifurahia sana kuolewa na George, kila siku alimshukuru sana Mungu kwa kumpa mume mkristo na mwenye haiba na tabia nzuri, ni furaha iliyoje atakayo kuwa nayo katika maisha yake yote! Baada ya miezi michache, siku moja Betty alijikuta akimwuliza Mungu, “kwa nini ulinipatia mume na kwa nini awe huyu?” Betty alikuwa amegundua kuwa George alikuwa hapendeki mda wote kama ambavyo angetaka. Hivyo hisia za Betty zikaanza kufifia moyoni, lakini baadaye  Betty alikumbuka maneno ya mchungaji siku ile ya arusi, “Unaahidi kumpenda mwanaume huyu?” Ndipo akajibu, “Ni lazima nimpende George! Ni lazima ni mpende hata nyakati anaporinga na kutoafikiana nami na kuonyesha ubinafsi, nategemea naye atafanya hivyo hivyo na kuendelea kunipenda hata kama nitaonyesha jeuli na ukaidi mara nyingine.” Halafu alijiambia, “kuanzia sasa nitampenda mume wangu na nitampikia chakula akipendacho!” Na alipokuwa anapika hisia zake za mapenzi zilianza kubadilika na alinza kujisikia kumpenda kwa mara nyingine. Ni kitendo cha upendo kwa mwanamke kumpikia mume chakula akipendacho, maana  vitendo vya upendo hurejesha hisia za mapenzi. Bahati mbaya wanawake na wanaume wengi hawafahamu ukweli huu, wengi huamini kuwa hisia za penzi zinapotoweka basi penzi nalo linapotea kabisa.
                                               Mambo ya muhimu kuhusu upendo
Ø  Penzi ni kitendo, ni kitendo cha kumjali na kumfikiria mwenzi wako na kuwa mpole, muungwana, mwenye subira, na mengine mengi yanayofanana na hayo. Unaweza kupenda kama utachagua kupenda.
Ø  Hisia ni hisia tu, kwa hiyo huja na kutoweka.
Ø  Kama utachagua kutopenda kwa vitendo basi hisia za mapenzi zitapotea kabisa.
Ø  Kama hisia zako za mapenzi zitatoweka, zirudishe tena kwa kuchagua kupenda kwa vitendo.
                                           Jambo la tatu
                                             3: TALAKA
Editha alimwambia kaka yake, “Nataka kumpa mume wangu talaka, nataka apate uchungu sana! Kaka yake alimwambia, “Hilo ni jambo zuri.” Nitakueleza namna ya kumwuumiza kikamilifu. Hatua ya kwanza anza kufanya juu chini, kila njia kumfurahisha, mfanyie vitendo vya ukarimu, zungumza naye kwa heshima na upendo na acha kulalamika, mara atang’amua kuwa anakutegemea na hawezi kuishi bila wewe. Halafu hatua ya pili, mpe talaka! Hakika kitendo hicho kitamuuma sana!” Baada ya miezi michache alimtaarifu kaka yake kuwa ametekeleza hatua ya kwanza. “Vyema kaka yake alijibu, sasa ni wakati wa kumpa talaka” “Talaka!” sauti ya Editha ilijawa na mshangao. “Kamwe siwezi!” Nampenda sana siku hizi, penzi letu limekuwa bichi tena!” Editha aligundua kuwa vitendo vya upendo hurudisha hisia za mapenzi. Bahati mbaya ni kwamba baadhi ya wengi waliooana hawajui wala hawajagundua ukweli huu. Wengi hufikiria kuwa wamepoteza penzi lao na hakuna chochote wawezacho kufanya  kurudisha penzi lao, baada ya hapo hatua wanayo fikiria ni kupeana talaka tu, hatua  ambayo pia haiwezi kukupunguzia matatizo au changamoto katika  ndoa yako. Agizo la Mungu kwa wana ndoa ni kupendana na si kupeana talaka.
(1wakoritho 13:8, Yohana 15:17, Waefeso 5:25, Mathayo 19:9)
Kitu ambacho  unatakiwa kukikumbuka ni ile ahadi uliyo iweka siku ya arusi yaani kupendana mpaka mauti itakapo watenganisha. Huu ndio wajibu unaotakiwa kuutekeleza, kumpenda mwenzi wako kama ulivyo ahidi. Kupenda sio rahisi, lakini kwa kuwa uliapa kumpenda mwenzi wako kwa msaada wa Mungu  lazima utekeleze. Mara uanzapo kupenda kwa vitendo, utashangazwa na kujawa na furaha  kuona kuwa hisia zako zimerejea, utakuwa tena na hisia  za kusisimua na kushangaza, hisia zinazo weza kukufanya uimbe na kupiga kelele za furaha na kusema, “Nampenda kwa moyo wangu wote.” Baada ya hapo ni wazi kuwa hisia zako za mapenzi zitapanda na kuteremka. Wajibu wako ni kumpenda mwenzi wako kila siku bila kujali kuwa hisia zako ziko juu au chini siku hiyo. Kama utafanya kazi nzuri ya kupenda kwa vitendo hisia za upendo katika ndoa yako zitazidi kukua na kuendelea kuwa za kusisimua kadri miaka inavyopita. Daima kutakuwa na matatizo  ya hapa na pale, lakini vipindi vya matatizo vitakuwa vichache zaidi ukilinganisha na vipindi vya furaha. Si rahisi  kwetu kupenda maana tuna asili ya ubinafsi, ukweli ni kuwa mara nyingi huwatunajisikia kufanya au kusema vitu visivyo vya upendo. Mungu anajua jinsi ambavyo ni vigumu kupenda lakini ametuamuru kupenda  na hutupa nguvu tunayohitaji kuweza kupenda. Inahuzunisha kuona kuwa mamilioni ya watu duniani wanakataa kuwa hawahitaji msaada wa Mungu, huzania kuwa wanaweza kumdu maisha yao bila msaada wake, ni wazi kabisa kuwa hawezi kuwasaidia wale wanaofikiri kuwa hawahitaji msaada wake. Kitu kingine ambacho wana ndoa wengi  wamesahau  ni kuwa wanapaswa kumwamini Mungu ili awasamehe dhambi zao na kupewa uwezo wa kutii amri amri za Mungu hii ni pamoja na kupenda. Kupenda si rahisi lakini kama tutaanza kwa kumpenda Mungu kwanza tunaweza kuanza kushinda vita hiyo, kwa sababu nguvu ya roho mtakatifu imo ndani yetu. Watu wengi husema, “kama utachagua kwa  uangalifu mwenzi wako wa ndoa, basi kupenda kutakuwa ni kazi rahisi,” lakini ukweli ni kwamba si kazi rahisi kupenda kila siku, mwaka hadi mwaka, upendo unahitaji juhudi, lazima tuweke jitihada katika kupenda kwani kupenda ni kazi. Kwa mfano: Mvulana anapovutiwa na msichana Fulani huwa mwangalifu sana, mpole na mkarimu kwake. Na iwapo huyu msichana anvutiwa na mvulana huyo na anataka naye apendeke, hufanya jitihada awe wa kuvutia, mcheshi na mara nyingi hujaribu kuepukana na haisira na kuwa mvumilivu na mwenye kujaa subira, vitendo hivi vya upendo huendelea kwa miezi kadhaa, baada ya hapo huoana………nini hutokea baada  ya kuoana? Mke hufikiria moyoni, “sasa nina mume; sina wasiwasi wa kuishi maisha yangu yote bila kuwa na mume, naweza kupumzika sasa.” Kulegea au kupumzika maana yake nini? Ina maana kuwa hajali tena kama anampendeza au hampendezi mumewe. Mume naye hufanya hivyo hivyo, badala ya kuwa mwangalifu na mwenye juhudi kufikiria mahitaji ya mwenzi wake, huanza kuzembea. Kinachotokea baada ya hapo, mmoja wapo anapoumizwa rohoni kwa maneno au kitendo Fulani, hatajaribu kusamehe wala hawi mwangalifu na husema maneno ya ukali ya kumuumiza mwenzi wake bila kujali madhara yatakayo tokea badaye. Kukumbuka kuwa ndoa yenu inaweza kuwa nzuri tu pale mmoja wenu atakapochagua kuwa mnyenyekevu na mkarimu hata hata kama hatendewi ukarimu na mwenzi wake, hii si kazi rahisi ndio maana wengi hawaifanyi, wako mapumzikoni, mara hisia za mapenzi huanza kupungua, lakini kabla ya kuoana kila mtu alikuwa mwangalifu kwa kumtendea mwenzi wake kwa ukarimu na hisia zao za mapenzi zilikuwa za kusisimua. Ili uhusiano wenu uendeelea  kuwa mzuri na nyakati zenu za kwenda kitandani zijae mapenzi ya kusisimua lazima mchagua kufanyiana wema kila siku, yaaani kufanyiana vitendo vya ukarimu.
                                                  Jambo la nne
                                             4: JINSI YA KUPENDA
Tumeona mambo mengi juu ya upendo na hisia za mapenzi, na jambo kubwa kati ya haya yote ni kumpenda mwenzi wako hata kama haujisikii kufanya hivyo, lakini swali hapa ni kwa njia ngani utaonyesha huo upendo wako kwa mwenzi wako kila siku?
                                       Njia ya kwanza
                       (a)Kuongea maneno ya shukrani 

Kila mtu aliyeumbwa na Mungu anahitaji kuthaminiwa, sote tunapenda kusikia maneno haya, “Nakupenda, nafurahi kuona unajitoa kunihudumia, nashukru kuona unawapenda wazazi wangu, una roho mzuri, na furahi kwa kuwa unanipenda, nina furaha kuolewa na wewe, kila mtu anahitaji kuishi na  mtu mwenye utajiri wa maneno kama haya.
Kama watu hawatupi shukrani  basi tunajisikia vibaya na kuumia rohoni, Neema alisema, “Mume wangu haonyeshi kujali kama nyumba ni safi, na mashati yake yamenyooshwa, yeye anachojua ni kuuliza kama chakula kikotayari,” Tunawajibika kujali na kuonyesha shukrani kwa wenzi wetu katika kila kitu wanachokifanya, siyo tu katika faragha bali hata hadharani. Ni furaha iliyoje kupokea shukrani mbele ya marafiki! Wambura na Roda waliwatembelea ndugu zake na mume, Roda limwomba mumewe, “Tafadhali naomba unipeleke dukani mara moja kwa gari, nataka kununua nepi zaidi kwa ajili ya mototo kwani zilizopo hazitoshi.” “kwa nini hauwezi kupangilia mambo yako vizuri!” Wambura alijibu kwa ukali, “ni lini utajifunza kupangilia na kuandaa mambo yako kabla ya wakati?” Wambura aliyasema haya maneno mbele ya ndugu zake….ambao Roda alikuwa amepania kuwaonyesha jinsi ngani alivyo mke mzuri. Fikiria jinsi gani Roda angefurahia kama mumewe angetafuta neno lolote zuri la kumsifia mkewe mbele ya ndugu zake! Wambura alipoteza nafasi nzuri ya kumpenda mkewe kwa maneno ya shukrani. Je, si udanganyifu kujaribu kumsifia au kumshukuru mwenzi wako hata kama haujisikii kufanya hivyo? Si kosa, maana Kutoa shukrani ni njia mojawapo ya kupenda na hakuji kwenyewe ni lazima tutie juhudi hata wakati ambao hatujisikii kufanya hivyo. Kama utampenda mwenzi wako wa ndoa kwa kumwonyesha shukurani,basi atabadilika na kuonyesha maendeleo mazuri! Lawama na malalamiko hiviwezi kumbadili mwenzi wako, lakini shukrani inaweza. Jaribu utaona matokeo yake!
                                      Njia ya pili
                     (b) Kufanya vitendo vya uungwana na ukarimu
Njia ya pili ya kupenda kwa vitendo ni kufanya vitendo vya uungwana na ukarimu, mwanzo wa ndoa yenu pengine ulikuwa mwangalifu kufanya vitendo vya uungwana na ukarimu kwa mwenzi wako, je bado unafanya hivyo mpaka sasa? Kumbuka Mungu amewaamuru waume na wake kupendana, na moja ya sehemu muhimu ya upendo ni kufanyiana vitendo vya ukarimu na uungwana, haya ni baadhi ya mapendekezo ya namna ya kutekeleza.
                                                                 WANAUME
                                                          
                                                          
Ø  Mweleze mkeo; “Nakupenda” halafu toa sababu maalum utaona uso wake unang’aa mara tu utajapo kitu kinachokufurahisha kuhusu yeye.
Ø  Nendeni matembezini pamoja, hii itamwonyesha bado ungali unapenda kutumia muda pamoja naye; Unastarehe ukiwa pamoja na mkeo.
Ø  Kila mara inapowezekana mletee zawadi mkeo, japo zawadi ndogo tu, mfahamishe kuwa zawadi hii ni kwa sababu, “nakupenda sana moyoni mwangu” nategemea unilipe kwa njia maalum usiku tuendapo kitandani”
Ø  Uwe mwangalifu unapoongea naye wakati umekasirika
Ø  Waeleze wazazi wake jinsi gani unavyomthamini binti yao.
Ø  Tumia muda kukaa na kuongea na mkeo, mfahamishe mawazo na hisia  zako.
Ø  Wajulishe wanao kuwa unampenda mama yao, waache waone matendo yako ya ukarimu na uungwana, wanapotambua unavyomtendea vitendo vizuri, watamheshimu….watakuheshimu na wewe
Ø  Tumia mda kuomba pamoja naye, kwa pamoja wekeni matatizo yenu mikononi mwa Mungu.
                                                      WANAWAKE
Ø  Mume wako anaporudi kutoka kazini, mpokee kwa tabasamu pamoja na maneno ya furaha na uchangamfu; ambayo yataonyesha furaha uliyonayo kwa kumwona. Usimpokee nyumbani ukiwa umenuna na umeekuja uso; badala yake fanya uso wako ung’ae na wenye furaha ukifikiria umuhimu wa mumeo.
Ø  Anapofanya kitendo Fulani kizuri mshukuru! Maneno mawili mazuri kuliko yote ya upendo ni “Asante sana”
Ø  Waeleze wanao  jinsi ambavyo unamthamini baba yao, siku moja Moringe alirudi nyumbani kutoka kazini kachoka taabani. Binti yake mdogo akasema, “Baba mama husema kwamba unafanya kazi kwa bidii sana ili kusudi tuishi vizuri hapa nyumbani.” Ghafla alisahau uchovu wake wote aliokuwa nao.
Ø  Vaa nguo  aipendayo na mfahamishe kwamba umeivaa nguo hiyo kwa sababu tu ni nguo anayoipenda sana.
Ø  Tafuta sifa zake nzuri na uzitaje mbele yake mara kwa mara.
Ø  Mara nyingine asubuhi; akiwa angali amelala, mletee kifungua kinywa kitandani; ukitumia vyombo vyako maalumu, weka sinia lako kitandani, ukiwa umevaa nguo yako maalum ya kulala ambayo inaonyesha mwili wako; na mwamshe kwa busu, kwa busu hilo tabasamu halitamtoka usoni siku nzima.
Ø  Kama utasikia mtu anasema kitu chochote kizuri kuhusu mumeo mweleze, usisite ukidhani labda mumeo atajivuna.
Inawezekana haujapendelea baadhi ya mawazo haya, hili si tatizo unaweza kufuata njia yako na maoni yako uyapendayo mwenyewe  kulingana na tabia, mwenendo na mila yako. Itakuwa  vizuri kama kila siku utapanga kitendo maalum cha ukarimu ambacho utamfanyia mwenzi wako wa ndoa. Hii inataka juhudi na nguvu ya kutekeleza. Ukweli ni kwamba kupenda ni kazi ngumu, lakini hufanya nyumba iwe na furaha na msisimko  wa mapenzi wa hali ya juu.
                                                             Njia ya tatu
                                     (c) Mkubali mwenzi wako kama alivyo
Njia ya tatu ya kupenda kwa vitendo ni kumkubali mwenzi wako kama alivyo, hata kama anamapungufu kadhaa. Ni wazi kuwa kuna mambo mengine hatuwezi kuyakubali katika ndoa. Kwa mfano, mwenzi wako wa ndoa anazini, huwezi kunyamaza na kumwachia aendelee kufanya hivyo, badala yake chukua hatua Fulani kuzuia kitendo hicho. Au kama mwenzi wako hukupiga, hauwezi kuvumilia tabia ya aina hiyo. Pamoja na hayo sasa,  katika ndoa kuna mambo mengi ambayo lazima tuyakubali, Christina alisema katika miaka mitano iliyopita amekwisha mweleza mume wake zaidi ya mara elfu moja kwamba asiache magazeti sebuleni, lakini bado anarudia, maana kila atokapo kazini huyasoma na kisha huyadondosha sakafuni, mpaka Christina ayaondoshe……...kitu cha kufanya katika hali kama hii, ni kwamba kila mtu katika mahusiano anapaswa kutambua kuwa anawajibu wa kumpenda mwenzi wake, hii ina maana kumkubali kama alivyo, uwe mcheshi na mkarimu kwake hata kama anarudia makosa ya yale uliyokwisha mweleza kuwa hayakupendezi, kwa maneno mengine ni kwamba…….Upendo huvumilia kasoro nyingi. Ukisema unampenda mwenzi wako maana yake umemkubali kama alivyo pamoja na udhaifu wake. Kisaikolojia wamaume hawapendi kuelezwa jambo la aina moja tena na tena, ukifanya hivi utaonekana kama unampigia kelele,lawama au aina Fulani ya mizozo. Kupiga kelele au lawama siku zote hazkumbadilishi mwanaume, badala yake hutamani kukimbia.
Ni afadhali kukaa katika pembe ya dari ,kuliko kukaa katika nyumba pana pamoja na                                            mwanamke mgomvi……….(mithali 25:24)
Badala ya kuwa mgomvi au kulalamika saa zote, ni jukumu la kila mtu katika mahusiano kumpenda na kumkubali mwenzi wake kama alivyo. Kama utafanya hivyo utagundua kuwa mwenzi wako anafurahi kuwa na wewe. Mara zote ni vizuri kama utaona udhaifu au kasoro Fulani kwa mwenzi wako, usilalamike au kuwa mgomvi, badala yake mweleze mwenzi wako kwa njia ya upendo jinsi gani ungependa abadilike. Baada ya hapo, kila uonapo hatua ndogo ya maendeleo onyesha shukrani na mpongeze, hata kama hautaona maendeleo yoyote, endelea kumpenda na kumkubali mwenzi wako kama alivyo. Hii itawafanya nyote kwa pamoja kuwa wenye furaha zaidi kwenye mahusiano yenu. Jaribu kufanya hivyo utaona! Pengine unafikiri, “Yote haya ni juu ya kupenda kwa vitendo, ni mawazo mazuri kwa baadhi ya watu.” Ni rahisi kusema: Badala ya kumkosoa mwenzi wako, mwonyeshe shukurani, mpongeze na mkubali hata kama ana kasoro. Kitu kikubwa hapa ni kwamba haupaswi kuwa na wasiwasi kuhusu nini mwenzi wako atakutendea, amua kumpenda mwenzi wako hata kama inaelekea unapata upendo kidogo kutoka kwake.
Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi,mwapata thawabu gani? (mathayo 5:25-25)
Usiseme kuwa haiwezekani, unaweza kumpenda mwenzi wako, siyo kwa nguvu zako ila kwa msaada wa  roho mtakatifu. Anza kwa kukiri mbele za Mungu kuwa umekuwa ukishindwa kumpenda mwenzi wako kwa vitendo, kubali kuwa siyo mwenzio peke yake aliyeshindwa kupenda, bali na wewe vile vile umeshindwa. Ungama sehemu maalum uliyoshindwa. Amini kwamba mwenyezi Mungu amekusamehe kabisa kwa sababu Yesu aliteswa na kufa msalabani badala yako. Kisha mpende mwenzi wako, onyesha shukrani, fanya vitendo vya ukarimu, acha kumkosoa mwenzi wako na anza kumkubali kwa upendo.
                                                         Jambo la tano
                                                   5: MAWASILIANO
Ndoa nyigi zimepooza na kuwa za upweke kwa sababu ya kukosa mawasiliano ipasavyo. Kuwasiliana maana yake ni kuongea kati ya wapenzi kwa uaminifu na uhuru. Endapo watu wawili wanawasiliana vizuri basi huongea pamoja juu ya matatizo yao yote, furaha, majonzi, na mawazo mbalimbali. Kama mume na mke hawawasiliani, ndoa yao huwa kama watu wawili wasiooana kuchangia nyumba moja. Tendo la ndoa huwa si kitu zaidi ya mume kuridhisha shauku yake na kutengeneza watoto, Ni lengo la Mungu, kwa  mume na mke kuwasiliana, wakati biblia inaongelea juu ya ndoa ya kwanza, inasema hivi.
Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe,wala hawakuona haya, (mwanzo 2:25)
Neno uchi lina maana, a) Hawakuficha miili yao kati yao. b) Hawakuficha mawazo na mioyo yao kati yao, waliwasiliana bila kufichana chochote. Baada ya hapo dhambi iliingia duniani, tokeo la kwanza la dhambi ni mke na mume kufichana, walitumia majani kutengeneza nguo ili waweze kujificha kati yao mbele na mbele za Mungu, hadi leo hii sisi binadamu tungalitunajificha, tunafichana hisia zetu za ndani. Wakati mwanaume anahisi anaweza kupoteza kazi yake hawezi kumweleza mtu yeyoyote,hufikiria watu watamdharau kwa kuogopa kupoteza kazi. Hivyo hujifanya kutabasamu na kuongea juu ya mpira wa miguu au hali ya hewa. Kila mmoja wetu anataka kuongea kuhusu anavyojisikia moyoni mwake, tunahitaji kuonyesha tunavyojisikia hali zetu halisi kwa wengine, ndio maana wote hupenda kuwa na marafiki japo hata mmoja. Tunahitali rafiki wa kweli ambaye tunaweza kuwasiliana waziwazi bila kuogopa. Kama mke na mume hawatimiziani mahitaji yao ya kuwasiliana, tendo la ndoa la ndoa litakuwa baridi na lisilo na msisimko.
                                         NGAZI ZA MAWASILIANO
Kuna viwango vitatu vya mawasiliano, na lengo la wanandoa linatakiwa liwe kufikia ngazi ya tatu. Ni vizuri kuanza na ngazi ya kwanza na baada ya hapo ngazi ya pili na tatu. Mke na mume wakifikia ngazi ya tatu hupata furaha isiyo kifani ya kuwa marafiki wa karibu, vile vile wakiwa wapenzi.
                                              Ngazi ya kwanza
                                        1: KUONGEA JUU YA MATUKIO
Mawasiliano rahisi na mepesi ni kuongelea juu ya mambo yaliyotokea siku hiyo, kwa mfano; mume unaweza kurudi toka kazini na ukamwelezea mke wako juu ya mkuu wako wa kazi ambaye alikuwa amelewa siku hiyo, na mke ukamweleza mume wako jinsi ulivyofanikiwa au ulivyoshindwa kuoka keki. Kuongelea juu ya matukio ya siku nzima ni mawasiliano mepesi na rahisi  kuliko yote, kwa bahati mbaya , pamoja na kuwa rahisi, watu wengi walioona hushindwa kuwasiliana hata katika ngazi ya kwanza. Wanapokutana jioni huwa hawana lolote la kuongelea, kama wewe na mke wako mna tatizo la aina hii, ni vyema kumwomba Mungu awasaidie, na baada ya hapo anzeni kuongea! Kila siku ongea na mwenzako juu ya jambo lililokutokea siku hiyo. Hapo mwanzoni itaonekana kama ni kazi nzito sana, lakini baada ya wiki chache kupita itakuwa mazoea mazuri ambayo nyote mtayafurahia. Pamoja na kumweleza mwenzio juu ya matukio ya siku nzima ni muhimu umwonyeshe mwenzio kuwa uko tayari kumsikiliza jinsi siku yake ilivyokwenda. Unaweza kufanya hivyo kwa kumwuliza maswali, maswali ni muhimu katika mawasiliano. Kama mume anarudi nyumbani na mke haulizi “mambo yaliendaje?” basi inaelekea mke hajali, na kama mume haulizi kamwe juu ya siku yake, mke naye huhisi mumewe hampendi tena. Sote hupenda kuulizwa maswali yanayotuonyesha kuwa wenzetu wanatujali, endapo mtu ataniuliza maswali kuhusu kazi yangu  au maoni yangu, huwa nafikiri hivi, “huyu ni mtu mzuri” katika ndoa vile vile tunapaswa kutumia maswali kuonyesha kuwa tunajaliana. Kuuliza na kujibu maswali juu ya matukio ya maisha yetu ya kila siku ni mwanzo  mzuri wa kuwasiliana; lakini msiishie hapo, pamoja na msaada wa Mungu mnaweza kupiga hatua na kufikia hatua ifuatayo.
                                                              Ngazi ya pili
                                                      2: KUONGEA JUU YENU 

Ngazi ya pili ya mawasiliano ni kuongea juu yenu: mipango yenu ya baadaye, ndugu zenu, fedha zenu na kadhalika. Kwa mfano, mume inamlazimu kujadiliana na mkewe maswali kama haya: Shule gani tuwapeleke watoto wetu?, Je, tumwombe binamu yangu kuishi nasi?, Je, tununue gari jipya au tujenge nyumba yetu? Mnapozungumzia juuu ya masuala yanayowahusu na yanayohitaji uamzi, mnaweza kukuta kwamba hamuafikiani katika mambo Fulani, hata kama ni hivyo msiruhusu kutokuafikiana kusimamishe mawasiliano yenu, badala yake ni lazima muendelee kujadiliana juu ya swala hilo hadi mufikie mwafaka. Mwanzoni Mwa ndoa ya Goodluck na Frida walizozana juu ya mama yake na Goodluck, na walifanya kosa kuacha mjadala huo bila maafikiano, na baada ya hapo  ili kuepuka mzozo  zaidi, wote walianza kuwa wangalifu na kujaribu kuepuka kutaja suala la mama yake na Goodluck. Baadaye tena walizozana kuhusu fedha, kwa mara nyingine tena mzozo huo haukutatuliwa ipasavyo, hivyo walianza kuepuka suala hilo vile vile. Baada ya miaka kadhaa walijikuta wanaorodha ndefu ya masuala ambayo kamwe kamwe hawakudhubutu kuyataja kati yao, swala kama hili hupunguza kiwango kikubwa cha mawasiliano katika mahusiano, usiruhusu mizozo inadhoofisshe kiwango chenu cha mawasiliano, hivyo ni bora kutumia mawasiliano kutatua mizozo yote inayowakabili. Mnaweza kufanya hivyo kama mtanuia na kuendelea kujadiliana juu suala hilo kwa njia ya upole na ya upendo na kupinga hatua hadi kufikia mwafaka kati yenu na kupata uamzi. Mnapo tatua mizozo yenu huwa ni rahisi kuwa huru kuzungumzia swala linguine lolote linalojitokeza baina yenu. Kwa njia hiyo mtakuwa tayari kupiga hatua kufikia hatua ya juu kuliko zote katika mawasiliano.
                                                    Ngazi ya tatu
                                              3: KUONGEA JUU YA HISIA ZENU
Katika ngazi hii ya mawasiliano mnachopaswa kufanya hapa nikushirikishana hisia zenu, kwa namna ambayo inakufanya ufungue mlango wa moyo wako kumruhusu mwenzi wako kuona kilichomo ndani, hivyo kukujua kiikamilifu jinsi ulivyo. Benja alimwambia mkewe, “leo kaka yangu alichukia na kunigombeza, isitoshe baba yangu naye alikuwa upande wake.” Taarifa ya tukio ni ngazi ya kwanza ya mawasiliano. Baada ya hapo Benja na mkewe wakajadiliana namna tatizo hilo la ndugu linaweza kutatuliwa, mazungumzo hayo yalikuwa ngazi ya pili ya mawasiliano, baada ya hapo mkewe akamwulinza Benja, “lakini unajisikiaje kuhusu kaka na baba yako?” Benja alijibu kuwa na wasiwasi moyoni kwa sababu ana hofu uhusiano wa familia unaweza kuharibika. Kushirikisha hisia namna hiyo ni ngazi ya tatu ya mawasiliano, ndoa huwa nzuri ajabu kama wana ndoa watafikia ngazi ya tatu ya mawasiliano. Mnapowasiliana katika kiwango hicho, furaha yenu huwa mara mbili kwa sababu furaha ya mmoja huwa ya mwenzie, na matatizo yenu hugawanywa kati na hupungua hadi nusu.
Haruni anadai kuwa yeye ni mkiristo halisi na kila mara huhudhuria kanisani pamoja na mkewe, lakini kila anapokuwa na tatizo hujiambia. “Sitaweleza mke wangu jinsi gani najisikia kuvujika moyo leo, mimi ni mwanaume hivyo mke wangu asije akafikiri siwezi kumudu shida” niwazi Haruni alisahau kifyngu kisemacho……… “Si vema mtu awe peke yake nitmfanyia msaidizi wa kufanana naye.” (Mwanzo 2:18)
Mwanaume yeyote asione aibu kuchangia hisia zake na mwenzi wake, maana kufanya hivyo hakutamsababisha azarauliwe na mkewe, badala yake ataheshimika na atajisikia huru zaidi kuchangia hisia zake na mkewe. Wanandoa wanaposhirikiana hisia zao wanakuwa wanawasiliana katika kiwango cha juu kabisa, na ndoa yao huwa ya kusisimua nay a kufurahisha ikiwaleta karibu sana kama pete na kidole.
                                                  VIKWAZO VYA MAWASILIANO
                                                           
Nijambo la kusikitisha kwamba ndoa nyingi zimeshindwa kuwasiliana katika ngazi ya tatu na baadhi yao hushindwa kufikia angalau ngazi ya kwanza, sababu kubwa hapa ni vikwazo ambavyo husimamisha mawasiliano. Na baadhi ya ndoa huruhusu vikwazo hivyo kusimamisha mawasiliano yao moja kwa moja. Vifuatavyo ni vikwazo vya mawasiliano.
a) Woga
Biblia inasema jukumu la mke ni kumheshimu mumewe, na siyo kumwogopa
      Ninyi wake , watiini waume zenu, kwani ndivyo apendavyo Bwana” (wakoritho 3:18)
     “Katika pendo hamna  hofu, lakini pendo lilillo kamili huitupa nje hofu {1 Yohana 4:18}
Kwa bahati mbaya kuna waume wengine huwafanya wake zao wawaogope, woga ni adui wa mawasiliano, na mume na mke hawawezi kuwasiliana ipasavyo kama mke anamwogopa mumewe.


b) kutosikiliza
Mawasiliano hayawezi kuwepo kama hauko tayari kumsikiliza mwenzi wako anapoongea, yaani kusikiliza kwa makini! Ni vizuri wakati mwenzi wako anaongea ufikirie maneno ya kumjibu baada ya yeye kumaliza kuongea. Ilikumfanya mwenzi wako ahisi unampeenda kwa kutilia maanani anachoongelea na kumsikiliza kwa makini, na baada ya hapo kama hauna uhakika anachomaanisha, ni wajibu wako kuuliza; Je, una maana kusema….?, hakika kusikiliza kwa makini ni kazi, lakini unalazimika kufanya kazi na ukishindwa kusikiliza kwa makini, basi utamvuja moyo mwenzi wako.
c) Kazi nyingi
pamoja na kuwa na kazi nyingi, ni muhimu mume na mke kutenga mda kwa ajili ya mazungumzo baina yao.
         d) Wajibu wa baba na mama    
                                                         
Mwanzoni mwa ndoa ya Yassin na Glory kwa hakika walifurahia kuwasiliana baina yao, kila mmoja wao alijisikia ni furaha ilioje kuwa na mwenzi wa ndoa ambaye unaweza kuongea naye juu ya jambo lolote lile. Lakini baada ya kupata watoto, Glory alikuwa akishughulika na malezi ya watoto, Yassin naye alikuwa kazini ili achume fedha kwa ajili ya kutunza familia. Watoto walichukuwa mda wao mwingi kiasi kwamba walianza kuzorotesha mawasiliano kati yao, hivyo uhusiano wao ulianza kupooza na kuwa baridi  usiokuwa na msisimko. Ndoa za aina hii ni nyingi hata katika nyumba ambazo mume na mke ni wakristo, lakini kwa hakika huo sio mpango wa Mungu, kwamba mume azingatie tu harakati za kutafuta fedha kiasi cha kukosa mda wa kuwasiliana na mkewe, vivyo hivyo na mke naye hapaswi kuegemea kwa watoto na kukosa mda wa kuwasiliana na mumewe.
                                          c) kuumia moyo
                                                   
Moja ya vipingamizi vikubwa vya mawasiliano ni kuumia moyo, Wenzi wa ndoa wanaweza kuumizana moyo kwa urahisi, hata uchungu kidogo unaweza kusimamisha mawasiliano katika ndoa yako. Asubuhi moja wakati Kamuli anaelekea kazini, aliendelea kuwaza juu ya jambo ambalo Marco alikuwa amelisema asubuhi hiyo, ambalo lilimuumiza, hata hivyo halikumuumiza sana bali kidogo tu. Ukweli ni kwamba sio maneno ya Marco yaliyomuumiza bali jinsi ambavyo Marco alivyokaza sauti yake wakati anaongea. Pamoja na hayo, alivyoendelea kufikiria juu ya kuumizwa huko, uchungu moyoni mwake uliendelea kukua, na alikumbuka nyakati nyingine pia ambazo mumewe alikuwa amemuumiza. Alipokuwa njiani kurudi nyumbani toka kazini Kamuli aliendelea kujiuliza nifanye nini kuhusu kuumizwa huku? Naweza kusahau jambo hili. Hapana, kama nitafanya hivyo, mawasiliano yangu mimi na Marco jioni hii yatakuwa hafifu; na bado nitaendelea kuumia moyoni. Labda ni msubiri atamke, `samahani`. Hapana, hiyo, haiwezi kusaidia kwa sababu inawezekana asiwe ametambua kuwa ameniumiza rohoni., kuna jibu moja tu hapa. Lazima niongee naye kuhusu alivyoniumiza moyoni, lazima nimweleze jinsi ninavyojisikia, lakini nitazungumza naye kwa upole na kwa uwazi.” Jioni baada ya watoto kulala, Kamuli na mumewe walikuwa wamejipumzisha sebuleni,  kwa aibu, Kamuli alianza kuongea. “Mpenzi nafikiri inafaa nikujulishe kuwa niliumia moyoni leo asubuhi kwa jinsi ulivyoongea na mimi,  haikunipendeza. Ukweli ni kuwa nimejisikia kuumia moyo siku nzima. Lakini nimetambua kuwa haukukusudia kuniumiza, na sasa naona aibu swala dogo kama hili kunibughudhi kutwa nzima.” Na baada ya mazungumzo hayo Kamuli na mumewe walijisikia  marafiki zaidi, na penzi lao jioni hiyo lilikuwa zuri mno.
Ni vizuri wana ndoa kuwa waangalifu kuchangua mda sahihi na mahali panapofaa kumweleza mwenzi wako juu ya jambo linalokutatiza, na sio wakati wowote. Mda unaoofaa ni ule ambao mnakuwa mmepumzika, na siyo wakati ambapo mwenzi wako anakuwa amechoka au ana njaa. Mahali panapofaa ni pale mnapokuwa mmekaa wawili kwa faragha pasipo kusumbuliwa na kelele yoyote. Vilevile mtahitaji mda wa kutosha kumaliza maongezi bila kukatizwa. Ni  muhimu mume na mke kutilia juhudi katika kujenga mawasiliano kati yenu.

                             
  

                                                                                                                                                                         












                                                     
                                            

Friday, September 24, 2010

MAMBO YA KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA UAMZI WA KUOA AU KUOLEWA:


1:KUOA AU KUOLEWA KUNABADILISHA UHUSIANO WAKO NA WAZAZI WAKO:

ZABURI45:10-11,MWANZO 2:24,
Haiwezekani ukaolewa/ukaoa halafu utegemee uhusiaono wako na wazazi wako usibadilike,maana yake lazima kuwe na mabadiliko mahali pa kuishi lazima mabadiliko yawepo kuh
usu mtazamo wako wa maisha.Kama hautalitambua hili mapema litakusumbua sana utakapoingia kwenye ndoa yako,pia unaweza ukawa ulikuwa umezoea kuwashirikisha wazazi wako kutatua kila kitu kwa maongezi kwa kuwashirikisha wazazi wako,ukiingia kwenye ndoa unapopata shida au jambo fulani mtu wa kwanza kumshirikisha lazima awe mwenzi wako na sio wazazi wako.kibiblia mzazi hapaswi kuingilia ndoa ya mtoto wake kimaamzi hata kidogo.hii ni sawa na kusema kwamba unapswa kubadilika jinsi unavyoweka kipaumbele.Unapoamua kuoa/kuolewa wa kwanza sio mama yako wala baba yako bali ni mke/mume baada ya kristo.

Kama hauwezi kufikia maamzi haya basi ndani yako yakumpa kipaumbele mke/mume wako baada ya kristo basi haujawa tayari koa/kuolewa.Kabla haujawasahau watu wa nyumbani mwa baba yako mume wako hawezi kuutamani uzuri wako,ukitaka mume wako autamani uzuri wako lazima uwasahahu watu wa nyumbani mwa baba yako.pia kama haujaolewa/kuoa haupaswi kumtamani mtu,lakini ukioa unarusiwa kumtamani mkeo tu.

Biblia imeweka utaratibu mzuri kabisa na waajabu ya kwamba ili mume autamani uzuri wa mke ni lazima mke awasahau watu wa nyumbani kwa wazazi wake.Ndio maana unaweza kuona mtu anamke mzuri sana lakini hamtamani hata kama anajiremba kwa kiwango cha kikubwa,huu huwa ni wakati mugumu sana lakini ndivyo unavyotakiwa kufanya.

2:FAHAMU YA KWAMBA HIYO NDOA INAKUINGIZA NA KUKUUNGANISHA NA FAMILIA NYINGINE:
 
Watu wengine wakioa/kuolewa hufikiria tu uhusiano wao wenyewe,hii ni hatari sana,kumbuka mnapooana mnaziunganisha familia zenu na kuwa ndugu kuanzia wakati huo.Maana yake unapoamua kumchagua mwenzi wako unapaswa kuangalia na hali ya familia yake hii inakusaidia kujua kuwa unaingia kwenye familia ya aina gani na unapofika kwenye swala la namna hii kuna vitu vingi vya kuangalia,Mfano:unaweza kuoa kwenye familia ambayo ni wavivu-maana yake itakuwa kazi ngumu kumshawishi mtu wa namna hii ajishughulishe na maisha.Nimuhimu kuwafundisha watoto wetu kazi za kila siku majumbani mwetu.Pamoja na usafi pia nilazima uangalie maana kuna familia zingine zina sumbuliwa na magojwa ya kurithi na usipojua kitu cha kufanya itakusumbua sana.
    3:UKIAMUA KUOA AU KUOLEWA, WAKATI MWINGINE IMANI YAKO INAWEZA KUBADILIKA.

Wasomaji wa biblia wanamfahamu mtu mmoja aliyeitwa mfalme Sulemani (unafahamu ni kwa nini aliandika kitabu cha Mhubiri, maana alipoandika kitabu cha Mhubiri akasema, mambo yote chini ya jua ni ubatili mtupu). Biblia inatuambia wazi kabisa ya kuwa Mungu alimpa hekima ya ajabu, na wasichana wakatoka sehemu mbali mbali duniani kwenda kufuatilia ile hekima, walipoikuta hawakutaka kuondoka na wakabaki pale kwake.
 Kosa alilofanya Sulemani ni kwamba wale wasichana walikuwa wanakuja na miungu yao, na alikuwa anawakaribisha wale wasichana na miungu yao, anawapa na mahali pa kujengea vibanda vya miungu yao. Biblia inatuambia wazi kabisa, ilifika mahali wale wakina mama wakamgeuza moyo wake usiendelee kumpenda Bwana.
Kitabu cha 1 Wafalme 11:4 kinasema hivi: “Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”
Nimeona vijana wengi sana ambao wanakuwa moto sana kwenye wokovu kabla hawajaolewa au kuoa, wewe ngoja waingie kwenye ndoa  na wafuatilie baada ya muda, utakuta wengine wamepoa mpaka wameganda kama barafu!  Ukiwauliza ni nini kimewafanya wapoe kiroho kwa kiwango hicho - wanaweza wakashindwa kusema. Maana kuna watu wengine wanafikiri ni kuolewa tu na mtu yoyote kwa sababu tu anasema Bwana asifiwe, ibilisi Pia huwa anaweka na watu wa kwake huko ndani ya makundi ya watu waliookoka.
Na ukikaa na vijana utapata baadhi yao wanaosema, ukitaka kupata vijana waaminifu siku hizi nenda katikati ya waliokoka, kwa hiyo wanajifanya wameokoka. Akikufuatilia juu ya kuoana na ukimwambia mbona wewe hujaokoka, na ukamtaka kwanza aokoke ndipo mzungumze, utakuta baada ya siku chache kupita anajifanya ameokoka, lakini ni yakubabaisha  tu ili akupate. Nimekutana na watu wa namna hiyo, msichana anaolewa akishafika ndani, ndio kijana anamwambia, na Yesu wako na wokovu wako nauvua hapa hapa, mimi nilikuwa nakutafuta wewe, nimekupata basi!
 Nimeona! Sisemi kitu cha hadithi, ninasema kitu ambacho nimeona kwa macho. Ikiwa umefika katika hali hii basi, ni mpaka kifo kiwatenganishe, na alikwishawaambia wenzake kwamba Mungu amenifunulia; kwa hiyo hana ujasiri wa kurudi na kusema kweli nilikuwa nimekosea, yalikuwa ni mafuniko sio mafunuo! Akitaka kwenda kwenye maombi anaambiwa hakuna; akitaka kwenda kuhudumu anaambiwa hakuna; anataka kwenda ‘fellowship’, anaambiwa hakuna; kaa hapo ndani. Kwa hiyo inabaki kazi moja tu ya kuombea chakula na chai na kwenda kulala!
 Na ni kwa sababu huyu mtu hakufikiri sawasawa, hakukaa akaona jinsi ambavyo hili jambo linaweza likambadilishia imani yake kabisa. Wewe nenda kwenye maandiko, utaona ya kuwa ndoa inaweza ikakubadilisha. Ndio maana kuna watu wengine wanaolewa, na wengine wanaoa na wanabadilisha dini, hii sio kitu cha mchezo, ni maamuzi magumu sana kuyafanya.
Unapobadilisha imani yako unabadilisha msingi wako kabisa wa maisha yako; kwa hiyo ni lazima uamue jambo ya kuoa au kuolewa kwa uangalifu sana.
Lakini pia inaweza ikawa ni mkristo kwa mkristo wanataka kuoana, lakini fahamu kuoa au kuolewa kunaweza kukakubadilisha dhehebu lako la kikristo, ndio maana lazima mkubaliane juu ya jambo hili kabla ya kuingia kwenye ndoa. Nilikuta vijana wamekubaliana kuoana, kijana mmoja mlutheri, kijana mwingine mpentekoste. Mambo yakawa magumu sana kwao, walipofika masuala ya kujadiliana, juu ya imani zao.  Ilikuwa ngumu sana, mpaka wachungaji wao wakaingilia kati.
Walipokuja kuniona, nikawauliza mko tayari kabisa na mnataka kuoana? Wakasema, ndio. Wakati huo walipokuja kwangu walikuwa tayari  wameshaenda nyumbani kwao, wameshazungumza na wazazi wao, na kote huko na wakati wote huo hawakufikiria hilo jambo. Sasa imefika mahali mchungaji wa kanisa hilo la pentekoste hakubali msichana wake aolewe kwa kijana wa kilutheri. Nikamuuliza maswali yule msichana akashindwa kujibu.
Unajua wapentekoste hawabatizi watoto, walutheri wanabatiza watoto. Mnapooana matokeo yake ni kwamba watoto watazaliwa. Ni lazima hicho kitu ufikiri kabla hajasema ndio kuolewa, au ndio kuoa. Sio umekwisha olewa ndipo unasema watoto wangu hawawezi kwenda huko, - ulikuwa wapi toka mapema ili uliseme hili tatizo? Maana unaweza ukafikiri ni masuala marahisi, sio masuala marahisi.
Maana wengine wanalichukulia jambo hili kirahisi, wakati jambo lenyewe sio rahisi. Masuala ya kwenda kusali kanisa tofauti tofauti huku mmeoana  sio mambo rahisi. Nimeona watu wakisema hakuna tatizo maana tutaoana, lakini kila mtu wetu atakuwa anakwenda kanisani kivyake; sawa, ninyi mnaweza mkaenda kivyenu, na watoto je?  Labda kama hamna mpango wa kuzaa!
Maana niliona kwenye TV, mtu mmoja, - dada mmoja huko ulaya  amefuga mbwa akasema, tuliamua huku ndani tusizae watoto na badala yake  tumefuga mbwa badala ya mtoto, wamempa na jina, wamempa na chumba wamempa na kitanda, anasahani yake, na bajeti yake, ana daktari, wameamua wasizae na badala yake, wamefuga mbwa! Labda kama unataka kuelekea njia hiyo! Lakini kama unaingia kwenye ndoa na unajua utakwenda kupata mtoto, suala la mahali mnapokwenda kusali ni muhimu sana kulijadili na kuliamua kabla ya kuingia kwenye ndoa.
Usiende kupeleka vita kwenye ndoa yako ambayo haitakiwi kuwepo! Unajua kuna vita vingine tunavianzisha bila sababu, hata Yesu alijua, wakati saa yake ya kupigwa mawe ilipokuwa haijafika, alikuwa anawakwepa wale watu waliokuwa wamepanga kumpiga mawe. Sasa kama Yesu alikuwa anakwepa majaribu mengine kwa nini wewe unajitumbukiza? Saa ikifika ya jaribu kuja kwako utalishinda tu, kwa sababu umetengenezwa na Mungu uwe na uhakika wa ushindi, kwa sababu ukiwa ndani ya Kristo unashinda na zaidi ya kushinda.
Imeandikwa hivi katika kitabu cha Warumi 8:37; “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda”. Lakini majaribu ya kujitafutia, yanaweza yakayumbisha imani yako.
 Maana watu wengi sana huwa hawajiulizi hili swali mapema lakini nimeona likiwapa shida. Wengine hata imefika saa ya kufunga ndoa, ndio kwanza  wanaanza kujiuliza, ‘ndoa sasa tunakwenda kufungia wapi’, hilo sio swali la kujiuliza saa hiyo, utakuwa umechelewa! Wewe ulikuwa unajua kabisa mwenzako anasali mahali fulani, na wewe unasali mahali pengine, imefika saa mnataka kufunga ndoa mnaanza kujiuliza, tukafunge ndoa kwenye kanisa la nani, ikiishafika hapo mnaanza kushindana na kuvutana; na haifai mambo kuwa hivyo.
 4:UAMZI WA KUOA NA KUOLEWA NI MUHIMU UWE MWANGALIFU NAO:


Kama hujawa mtu wa kuwajibika, basi, hujawa tayari kuwajibika, kwa hiyo usiingie kwenye ndoa! Kuoa au kuolewa kunakufanya uwajibike zaidi, maana yake ni kutafuta wajibu mkubwa zaidi.
 1Timotheo 5:8 anasema, “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiye amini”, maana yake ni mbaya kuliko mtu ambaye hajaokoka. Afadhali mtu yule ambaye hajaokoka. Huyo ambaye ameokoka, lakini hatunzi watu wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, maana yake amemkana Yesu; ni mbaya kuliko hata mtu ambaye hajaokoka.
Hii inaonyesha ya kuwa  unaweza ukaingia kwenye ndoa ukapoteza wokovu wako, ukakosa kwenda mbinguni, si kwa sababu umefanya dhambi ya uasherati, lakini kwa sababu umeshindwa kutunza watu wa nyumbani mwako, na kwa ajili hiyo unahesabika kuwa umeikana imani.
Ukiangali kwenye Tito.2:3-5 anasema, Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu, wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema, ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao,  na kuwa wenye kiasi, na kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe, ili neno la Mungu lisitukanwe”.
Unaweza ukaona kabisa ya kwamba Timotheo, anazungumza habari za vijana wa kiume waliooa na wanafamilia, au umeoa na hujapata mtoto. Unao watu nyumbani mwako, inawezekana ni msichana umeolewa, huu mstari pia unakubana. Ukienda kwenye kitabu cha Tito, Tito anaandika moja kwa moja habari za wanawake wazee, ili wawasaidie wanawake vijana, maana yake wasichana ambao ndio wameolewa tu. Anasema, “Wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao”.
 Usingetegemea msichana aambiwe awapende watoto wao, hutaona mwanaume anaambiwa awapende watoto, bali anaambiwa awalee watoto. Mwanamke anaambiwa awapende watoto, ni kitu ninashangaa kila siku; maana nisingetegemea mama aliyepata uchungu wa kuzaa aambiwe ampende mtoto. Watu waliookoka wengi hasa wanapoingia kwenye ndoa, wanaingia kienyeji - kienyeji tu, hawajali ya kwamba kuna kuwajibika.
Huwa ninawaambia vijana siku zote, hata kama mlikuwa mmezoea kutokula nyumbani mwako, (maana kijana akiwa bado hajaoa, anaweza akakaa wiki au wiki mbili, jiko lake halijawahi kupika kitu); kijana akiwa bado hajaoa, hakimsumbui ana hela au hana hela, ataishi. Chakula kikiisha anaenda kutembelea ndugu na jamaa, kama hawataki kumpa chakula, atakaa hapo mpaka amekula na ndipo aondoke. Akikosa kabisa atajitia moyo kwa Bwana kwamba amefunga, na kumbe ameshinda njaa!
 Wakati mwingine mambo yakimzidia, na hana sabuni ya kufulia nguo anasema hajali, kwa hiyo anaendelea, hana shida, anabadilisha nguo sio kwa sababu amefua, lakini anabadilisha ili angalao jasho liweze kupungua hasa mnuko wake, kwa hiyo anaitundika mahali ipigwe upepo usiku; na baada ya siku mbili anavaa hiyo hiyo tena!
 Huwa ninawaambia vijana siku zote kama hauko tayari kuwajibika, usioe. Kwa sababu kama umeoa, haijalishi ya kwamba unafunga au hufungi, chakula lazima kiwemo nyumbani mwenu. h haleluya! Na ukishaoa tu, maana yake umeitangazia dunia nzima ya kuwa umeamua kuwajibika, na unaweza ukatunza mke. Mambo ya kwenda kuomba -omba msaada tena inakuwa ni kitu ambacho si wakati wake sasa. Maana unaposema, mimi nimeamua kuoa, maana yake umekubali kuwajibika –na hii ni pamoja na kumlisha na kumtunza mke wako.
Ndio maana ukienda kwenye makabila mengine wanakuambia, ‘kijana unataka kuoa umejenga nyumba?’  Nimeona makabila mengine wanauliza, ‘kijana wewe utaoaje wakati hata nyumba huna?’ Ndio maana vijana wanazuiwa kuoa wakiwa shule, kwa nini, kwa sababu katika ndoa watahitaji kuwajibika. Sio kwa sababu wakiwa shule hawawezi kuoa, ila ni kwa sababu wanajua suala la kuoa sio kitu cha mchezo, linahitaji mahali ambapo unahitaji kuwajibika. Ndani yako lazima uwe umekubali  kuubeba wajibu uliomo katika ndoa!
Na kama ni msichana unataka kuolewa ukubali kuwajibika basi la sivyo usikubali kuolewa kama hujawa tayari kuwajibika. Tito anawaambia wazi kabisa, ya kuwa  wafanye kazi nyumbani mwao wenyewe. Lakini sasa unataka hata kama umeolewa, uishi maisha kama msichana, na hiyo ni hatari sana. Ukiingia kule ndani ya ndoa kuna mabadiliko. Wakati ule ulikuwa unaosha vyombo vichache maana ni vya kwako peke yako, sasa na mume wako yuko, na marafiki zake wamekuja –vyombo vya kuosha vitaongezeka, na kuwajibika kwako kunaongezeka.
 Ilikuwa inakusumbua kupika, unapika mara moja kutwa, na siku hizi wataalamu wametuletea kitu kinaitwa ‘hot pot’, kwa hiyo hii mambo ya kupasha pasha moto chakula siku hizi wakati mwingine hayahitajiki. Mtu ameweka chakula chake anakifunika vizuri, anakuja jioni anakuta bado cha moto. Lakini ninakuambia labda umeingia umeolewa na mtu ambaye ni mtumishi, ana wageni nyumbani kwake kama kituo cha polisi, kila baada ya dakika mbili amekuja na wageni wengine.
Labda mume wako ni mkarimu sana, kila mgeni akija anakuambia, “fulani chai vipi?”  Huko jikoni ‘unauma vidole’ maana umeshaingia jikoni kuanzia asubuhi; labda saa hiyo ni saa tano, na umeshaingia jikoni kupika mara nyingi, maana wageni wanapishana kila wakati. Kila saa ‘chai, chai’, unatamani uondoke ili usiendelee kupika, lakini umebanwa – ndio kuolewa kwenyewe huko. Ukiamua kuolewa kuwajibika kwako jikoni kutoangezeka zaidi.
 Huwezi ukaamua tu saa yoyote ukasema, mimi nataka kwenda kutengeneza nywele, huo muda wa uhuru wa jinsi hiyo umekwisha, ukitaka kwenda kutengeneza nywele lazima uage, huwezi ukaondoka tu saa yoyote unayotaka, kila kitu kinabadilika. Kuna masuala ambayo utahitaji kuwajibika nayo pale nyumbani, huwezi kukwepa! Na kuna mambo mengine hakuna mtu mwingine ambaye atafanya kwa niaba yako; kama usipotaka kuyafanya wewe.
Ndio maana watu wanafika mahali, msichana anaolewa lakini wiki ya kwanza  tu anataka msichana wa kazi wakati, hana hata mtoto mdogo. Unataka msichana wa kazi wa nini, huo ni uvuvi tu. Lazima uwe mwangalifu, wewe umeolewa tu, unataka msichana wa kazi, wa nini? Unaweza ukajitetea na kusema ni kukusaidia kazi - kazi zipi? Unaweza ukajitetea na kusema, aa! Unajua ninachelewa sana kutoka kazini, angalao nikute mtu wa kupika.  Mimi ninakumbia unaanza vibaya. Kama ndiyo kwanza umeolewa tu, na unataka wakumpikia chakula mume wako awe ni msichana wa kazi, basi unaanza vibaya.
Wakati huo ndio saa ya kumtayarishia mume wako mapishi ambayo hajawahi kuona kwenye nyumba ya baba na mama yake!  Akikaa mwenyewe huku anakula awe anasema, ‘ahsante Yesu kwa kunipa msichana wa namna hii!’ Kwa sababu hajawahi kuona chakula kizuri cha namna hiyo ulichompikia -  hata hoteli hajawahi kukipata!
Lakini unaanza tu maisha ya ndoa na  kumbandikia mume wako watu wa kumhudumia, mimi ninakuambia unaanza vibaya, huko unakoelekea na ndoa yako sio kuzuri. Uamuzi wa kuoa au kuolewa usiucheezee, kaa chini, fikiri kwanza na kuomba kabla hujaamua.
5:UAMZI WA KUOA NA KUOLEWA,UNAWEZA KUBILISHA UTUMISHI WAKO NA WITO WAKO     KABISA; 
 
 Ngoja nikutolee mfano wa kibiblia. Unamkumbuka mtu mmoja aliyeitwa  Samson, alimwoa dada mmoja aliyeitwa Delila, utumishi wake ulinyongewa huko kwenye maisha yao ya ndoa. Ukisoma kile kitabu cha Waamuzi.16:21 kinasema hivi, “Wafilisti wakamkamata wakamng’oa macho, wakateremka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba naye alikuwa akisaga ngano katika gereza”.
Unajua huyu alikuwa ni mtumishi wa Mungu mzuri kabisa. Lakini hakujua ya kwamba yule mwanamke aliyempenda na akamwoa aishi naye alikuwa ni ‘ajenti’. Hakujua ya kuwa  yule dada alikuwa ni ‘ajenti’ wa adui. Yule dada alikuwa ni ‘ajenti’; kabisa akambembeleza mume wake amweleze siri ya nguvu zake, lakini Samsoni mwenyewe alikuwa anaficha kusema siri ya nguvu zake iko wapi. Lakini yule dada alikuwa na ujuzi wa kubembeleza. Akambembeleza yule baba kiasi ambacho akashindwa kuficha siri yake, na akaisema.
 Unajua inapofika kwenye masuala ya ndoa inatakiwa muweze kusaidiana, mtu asitumie udhaifu wako kukuangusha, mtu asitumie udhaifu wako kukuzamisha, mtu asitumie makosa yako kukupeleka jehanamu, inatakiwa ukimpata mwenzako ukiwa na udhaifu akusaidie, ukiwa kwenye dhambi akuombee utoke, unaelekea jehanamu akusaidie kwenda mbinguni, ndivyo inavyotakiwa iwe kwenye ndoa.
Lakini ninakuambia ukimpata mtu, na wewe una maisha yanayoelekea  jehanamu, anakuambia nenda salama, hii ni hatari. Yule dada alikuwa anamfuatilia Samsoni kumnyang’anya kitu kilichokuwa ndani yake cha utumishi alichokuwa amepewa na Mungu, na Samsoni hakujua. Alipofika mahali pa kuisema siri yake alifikiri mke wake  ni mwenzake ambaye anaweza akampa siri yake vizuri bila shida.
Ndio maana kwenye ndoa ambazo watu hawaaminiani vizuri, siri zao hawaambiani. Na ikishafika kwenye ndoa, mnasiri mlizozifichana iko shida, maana yake kuna eneo ambalo usingetaka liingiliwe, unafunga na ufunguo, kasha unatembea na ufunguo mfukoni. Ni eneo umeficha, kwenye ndoa mnatakiwa mfahamiane kila siku, na udhaifu wako, na shida ilioko, na matatizo yaliyoko, kila kitu kiwepo peupe, ili mwenzako atafute namna ya kukusaidia.
Samsoni aliona kitu cha tofauti, lakini alikuwa mke wake, maadui wakaja wakamshika, mke wake anatazama na kushangilia. Badala ya Samsoni kumtumikia Mungu, akaenda akawa anasaga ngano gerezani. Biblia inasema wakamtoboa macho.  Kwa jinsi ya rohoni ningekuambia, wanaondoa macho yako ya rohoni, maono ya Kimungu yanapotea, mtazamo wa Kimungu unapotea, mipango ya Kimungu inapotea.
Ndio maana unakuta mtu ameolewa ameokoka, au ameoa huku ameokoka, akifika ndani ya ndoa maono ya Kimungu yanapotea, na utumishi wake unazama.  Anabaki kusema ‘Bwana asifiwe’, kama bado anaweza akaendelea kusema ‘Bwana asifiwe’, lakini ndani ya moyo amenyonywa kiroho na hakuna kitu.
Sasa labda na ninyi ni mashahidi, wewe angalia vijana ambao wameoa na kuolewa, angalia kama bado wanao moto ule ule wa utumishi, ambao walikuwa nao kabla hawajaingia kwenye ndoa. Wengine wanabaki  kumsingizia Mungu ya kuwa, ameesbadilishia huduma, wakati sio Mungu, kumbe ni mume wake amembadilishia huduma, au ni mke wake tu amembadilishia huduma! Maana hakuhesabu gharama ya ndoa kwenye wito wake.
 Kwa mfano; Mke wako anakutaka nyumbani, huduma inakutaka kila siku uwepo barabarani, usije ukafikiri ni kitu kirahisi hicho. Utafika mahali lazima uamue, unataka kumpendezesha mke wako au unataka kumpendezesha Mungu.Haya si mambo ambayo ni rahisi kuyaweka vizuri na kuyaanisha bila msaada wa Mungu. Na kama alikuwa anajua anaolewa wapi, kusumbuliwa suala la kusafiri kwako kwenye huduma lisingekuwepo, angekua anakutia moyo na kukuombea, na kukusindikiza siku nyingine. Lakini inapofika anaanza kupata shida, maana yake kuoana kwenu kuna kasoro mahali, na kumekuwa mzigo.
6:UAMZI WA KUOA AU KUOLEWA UNAWEZA KUKULETEA MARAFIKI WENGI AU MAADUI:

Sasa nakufikirisha hivi vitu vikusaidie, inawezekana kabisa hujafikia umri wa kuoa au kuolewa, lakini ninakuambia weka maombi yako ya akiba, (sijui kwa upande wako, lakini mara nyingine huwa nawaombea watoto wangu maombi ya akiba, kwa ajili ya ndoa zao kama Yesu atakuwa hajarudi, kwa sababu najua maana yake ni nini).
 Ni vizuri upate maombi ya namna hii mara kwa mara - ujiombee mwenyewe, ukipata watu wa kukuombea shukuru Mungu, lakini hata kama hujapata watu wa kukuombea, ninakuambia kazana kujiwekea maombi ya akiba. Hiyo ni njia panda. Mahali pa kuoa au kuolewa ni njia panda. Ukichagua njia ambayo haiko sawasawa, maisha yako yatakuwa magumu sana.
Sasa ukiangalia kwenye kitabu cha Hesabu.12:1-2 inatuonesha wazi kabisa ya kwamba, harusi ya Musa ilileta ugomvi katikati yake na ndugu zake, hasa dada yake na Haruni. Kilichowasumbua ni kwamba alikwenda kuoa mwanamke Mkushi; au amekwenda kuoa mahali ambako hawakutarajia, kwa hiyo wakakasirika. Halafu naamini Musa aliwaambia Mungu amesema naye juu ya kuoa mke huyu, wale watu wakasema, ‘Mungu anasema na Musa tu peke yake, haiwezekani’ - ugomvi ukaingia.
Unajua ugomvi uliingia kiasi ambacho Mungu akasikia yale maneno na hayakumfurahisha, akawaita kwenye hema. Ikabidi ajieleze wazi uhusiano wake na Musa.
Kitabu cha Hesabu 12:6-8 kinasema; “Kisha akawaambia, Sikilizeni basi maneno basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?” Alivyomaliza kusema namna hiyo dada yake Musa akapata ukoma!
 Ugomvi umetokea wapi? Musa alipooa! Kwa kuwa ameoa msichana ambaye dada yake hakumtaka. Mungu alimtaka, lakini dada yake hakumtaka. Dada mtu akaanza kumsema kaka yake, Mungu akampa adhabu! Dada mtu alipopewa adhabu ile na kaka mtu akapata shida, Israeli nzima ikapata shida, hawakusafiri walisimama wote, hawakuendelea na safari. Ugomvi ulitokea wapi? Ulitokea mtu mmoja alipooa!
 Nimeona ndoa zingine kijana anaoa lakini uhusiano wake na baba yake na mama yake unakatika wakati huo huo. Vijana wengine wanakuwa hawako waangalifu hapo, na ndio maana mambo yakiwa magumu, na wazazi wanawabishia juu ya kuoa au kuolewa kwao  hawataki kwenda kuzungumza na wazazi wao; wanapiga ‘short cut’, wazazi wao wanakuja kuambiwa tu saa na tarehe ya harusi!
Biblia inasema, “waheshimu baba na mama yako, hii ni amri ya kwanza yenye ahadi ili upewe siku nyingi katika nchi upewayo na Mungu wako” (Waefeso 6:1). Na kwa sababu hiyo vijana wengi sana wakiishakorofishana wazazi wao hawaendelei katika ndoa muda mrefu wakiwa na amani.
Sasa sisemi kwamba wamkubali tu huyo msichana au huyo kijana, ni zaidi ya hapo unajua. Suala ninalozungumzia hapa ni la wao kukupa kibali, na wakafurahi. Unaweza ukasema, hawaelewi kitu au hawajaokoka, kwa hiyo hawahitaji kuelezwa kitu. Hapana!
Ndio maana unahitaji kuomba. Kwa sababu unajua suala la kutaka kuleta msichana au kijana ndani, sio la kwako peke yako, linawahusu wazazi wako na ndugu zako kwa sababu unawaingiza kwenye familia nyingine. Hata kama unataka kuoa au unataka kuolewa, ni mambo ya kifamilia maana ni koo mbili zinakutanishwa na kuunganishwa.
Wakati mwingine unaunganisha kabila mbili au unaunganisha kabila tatu, (wengine hawaelewi kitu ninachosema, kwa mfano;  “Mimi ni mnyakyusa, mke wangu ni msukuma, watoto wangu ni kabila gani”? Wanakabila mbili, ni mchanganyiko wa wanyakyusa na wasukuma, maana ningetaka kujipendelea ningesema ni wanyakyusa.
Lakini ndani wanaunyakyusa na wanausukuma halafu waolewe na mtu wa kabila lingine ambalo sio mnyakyusa wala sio msukuma, ni makabila mangapi yanaungana hapo, matatu! Sasa fikiria na anayeoa  kwangu na yeye  awe ametoka kwenye mchanganyiko wa namna hiyo.
Unaunganisha hapo makabila matatu, manne, matano, sasa wewe unataka wazazi wako wasiifuatilie ndoa hiyo kwa karibu. Kwa nini? Ukipata shida utarudi kwa wazazi wako, sasa kwa nini wakati wa maamuzi wasikusaidie!
 Na mimi ninakuambia iko njia ya kutokea, ikiwa utapata tatizo la namna hii; wewe kukaa kwenye maombi kwa namna ambavyo, kama ni Mungu kweli aliyekupa huyo msichana au aliyekupa huyo kijana, basi ataweka kibali hicho hicho ndani ya wazazi wako, ili na wao wamkubali.
Saa nyingine unaweza ukapata marafiki wengine wazuri, lakini wakati mwingine marafiki wengine wanakuwa ni wabaya. Maana ukishaolewa marafiki wa mume wako ni marafiki zako, ukishaoa marafiki wa msichana ni marafiki zako. Vijana siku hizi wanaotaka kuoa au kuolewa wakitaka kujua ukoje, hawakuangalii wewe wanaangalia marafiki zako. Marafiki ulionao ndio wanaoonyesha picha uliyonayo ndani yako.
Rafiki wa kweli hafuati pesa ulizonazo, anafuata tabia uliyo nayo, wale marafiki wanaokufuata kwa sababu unacho kitu cha kuwapa hao sio marafiki, wanakufuata kwa sababu unachokitu, siku ukiishiwa huwaoni. Lakini wale marafiki unakuwa nao wakati wa shida na wakati wa raha, ni marafiki ambao malengo yenu na tabia zenu, kufikiri kwenu kusema kwenu zinafanana. Hao ndio marafiki ambao wanakuwa marafiki zako wa kweli; siku ukiwa na shida ni marafiki zako, unahela ni marafiki zako, umefilisika ni marafiki zako, hao ndio marafiki zako!
 Sasa kama mtu anataka kukuangalia ulivyo, anaangalia marafiki zako. Sasa, akiangalia marafiki zako, hata kama unasema, ‘Bwana asifiwe’, hata kama unapiga pambio mpaka jasho la damu linatoka, lakini wanaangalia marafiki zako ulionao, na wakati mwingine ni wabaya kuliko wale wa kule duniani, wanajua na huyu msichana au huyu mvulana kuna mahali ‘ana short’.
Kwa wengine inakuwa vigumu kuliona kwa namna hii, lakini ni lazima ufahamu ukiwa kama kijana, lazima uwe mwangalifu juu ya marafiki ulionao. Vijana wengine wanabaki kushangaa kwa nini wasichana wanahangaika wanasema hatuoni vijana wa kuwaoa, wakati vijana wapo, lakini  nani ataolewa  na vijana ambao wameokoka lakini hawana msimamo? Nani anataka kijana wa namna hiyo ambaye anashinda vijiweni sawasawa na hao vijana wengine wa duniani?
Mwanaume akitaka kuoa lazima ajifunze kuwajibika. Hawezi akawa na marafiki ambao hawawajibiki kimaisha – na akataka aone na aendelee na urafiki nao. Akiwa karibu na hao marafiki, itakuwa ni vigumu kuwa na ndoa yenye amani. Angalia tu marafiki alionao, unashangaa kwamba anaendelea kusema bado ameokoka. Unashangaa wale marafiki alionao, hawafananii, hawawezi hata kumtia moyo kuomba, hawawezi kumtia moyo kusoma neno, vitu wanavyozungumza ni vitu vya ajabu.
Unajua, hata wakati mmoja  hawana maneno ya kutiana moyo ya kuwa na maendeleo binafsi, lakini ndio anaoshinda nao toka asubuhi mpaka jioni, halafu anataka kuoa msichana ambaye ameokoka, anayeshinda kwa Mungu , anayekaa kwenye maombi, anayetaka kuona cha Mungu kinasimama katika maisha yake, ndiye anataka kwenda kwake ili amuoe;- hii siyo sawa! Ndoa yao itakuwa na matatizo tu kwa muda mrefu.
 Maana usije ukapata shida ukiingia kwenye ndoa na kijana wa namna hiyo. Wewe uliona kabisa marafiki zake walivyo, unaolewa na ndipo unaposema, ‘mimi sitaki hao marafiki zako’! Imeanza wapi? Atakuambia vizuri kabisa “ulinikuta nao”, kwa nini hukusema mapema kabla hatujaoana ya kuwa huwataki?
Msichana anaolewa na ndipo kijana anamwambia hao marafiki zako nisiwaone hapa, lakini alikuwa anawakuta chumbani kwako wakati alipokuwa anakuja kukutembelea na hakusema kitu, na wakati mambo yakiwa magumu katikati yenu alikuwa anawatumia wao kukubembeleza ukubali kuolewa naye, sasa umekwishaolewa hawataki. Anaanza kuwasema ya kuwa  tabia zao sio nzuri. Hili jambo si zuri; alitakiwa aseme mapema juu ya kutoridhika kwake na rafiki zake.
 Unapotaka kuoa au kuolewa, usifikirie tu picha ya yule mtu wakumuoa au kuolewa naye, ni vizuri kuangalia na aina ya marafiki zake wa karibu – je unaweza kuchukuliana nao?.
7:JE UKO TAYARI KUOA AU KUOLEWA
 
       
Ni swali muhimu, uko tayari, maana yake umefika mahali hali yako ya ndani na nje, inakuruhusu kuoa au kuolewa? Uko tayari kuoa au kuolewa? Umefika mahali pa namna hiyo?. Wengine wanasema huyu ni mtoto, lakini unajua pamoja na kwamba ni mtoto, ni vizuri kujua kama uko tayari kiumri.  Lakini ninapozungumzia hapa juu ya utayari wa kuoa au kuolewa, sizungumzii tu habari za miaka, bali ninazungumzia habari za hali yako ya ndani.
 Nimeona kuna mtu mwingine ana miaka arobaini, lakini kwa kweli hayuko tayari kukaa na mwanamke, ndani yake, mawazo yake na kufikiri kwake, hayuko tayari kukaa na mwanamke, hawajibiki hata yeye mwenyewe juu yake mwenyewe. Wengine hata wana miaka hamsini, lakini ana hali kama hii. Nimeona akinadada hata wana miaka arobaini na tano, hayuko tayari kuolewa, maana akiolewa ni shida tu.
 Nilienda mahali fulani, nikakuta dada ana umri mkubwa tu, lakini wakati wa maombi hakusema kama anataka tuombe ili aolewe. Nikaona ngoja nimuulize labda anaona aibu kusema hitaji hili kwa sababu umri umesogea, nikamwambia “hutaki tuombe uolewe”? Akasema, “hapana, sitaki kuolewa” (Na alikuwa ana umri wa miaka kama arobaini na zaidi). Nikamuuliza, “kwa nini”. Akasema, “kwa sababu sitaki kuomba ruhusa kwa mwanaume ninapotaka kutumika”. Nikamuuliza unafanya kazi, akasema, “ndio”.
Nikamwambia, “unapokwenda kumtumikia Mungu huwa unafanyaje, - unaomba ruhusa au unatoroka huko kazini?” Akasema, “ninaomba ruhusa”. Nikwamwambia, “kwa nini unaona ni rahisi kuomba ruhusa kwa mwajiri wako na unaona taabu kuomba ruhusa kwa mume wako?” Alishindwa kujibu hilo swali. Nikamwambia tatizo lako ni kubwa kuliko unavyo fikiri.
Unaweza ukaona kabisa ya kwamba, huyu mtu hayuko tayari kuolewa, wala msijaribu kumlazimisha  aoelewe – pamoja na kwamba umri wake ni mkubwa. Usijaribu kumsukuma kwenye maamuzi ya kuolewa maana hayuko tayari kuolewa, akiingia kwenye ndoa atakwenda kuleta shida tu!
 Ndio maana ninakuuliza swali, je uko tayari kuoa au kuolewa? Lina vipengele vingi vya kulitazama, na linabadilisha vitu vingi sana.
Mwingine unakuta ni msichana, wazazi wake ndio wanamtegemea karibu katika kila kitu. Mimi ninakuambia kabla hujafikiria kuoa au kuolewa, fikiria hilo swali. Kwa sababu ukiishaolewa tu biblia inakuambia wasahau watu wa nyumbani mwa wazazi wako  (Zaburi 45:10). Sasa haimaanishi usiwasaidie, ila maana yake ni kwamba huwezi ukawasaidia tena ‘moja kwa moja’ kama ulivyokuwa unawasaidia zamani. Ni vitu lazima ujadiliane na mume wako juu ya kuwasaidia wazazi wenu wa pande zote mbili – maana mna mipango yenu sasa.
Na inawezekana labda umeoa au umeolewa kwa kijana ambaye hana mzigo na wazazi wake kabisa, kila mtu anaishi kivyake vyake kama simba  porini, suala la kusaidia wazazi hana ndani ya moyo wake. Wewe umekuwa na huo mzigo, wazazi wako wamekulea, umefika mahali umeanza kazi, sasa na wewe unawatunza hatua kwa hatua, siku unaolewa yule baba anasema basi usiwatunze tena,  - fikiri hilo.
 Litakuwa linakuumiza kila siku jinsi wazazi wako wanavyopata shida. Utafika mahali utakuwa unachukua vitu kisiri siri unapeleka kwa wazazi, na hiyo ina shida yake pia. Kwa hiyo kabla hujakubali kusema mimi nataka kuolewa, fikiri kwanza na kuomba, maana ndoa inakwenda kukubadilishia mambo yako mengi.
8:"JE UKO TAYARI KUOLEWA NA NANI"
 
Wengine hawafikirii namna hiyo, ukiwauliza uko tayari kuolewa na nani, anasema na mtu aliyeokoka. Bwana anawajua walio wake, hakuna mtu kwa jinsi ya nje atakayemjua mtu aliyeokoka kisawasawa hasa alivyo kitabia. Maana watu wengi sana wanasema wameokoka lakini hawajaokoka, wengine wanasema ‘bwana asifiwe’ lakini ni bwana mwingine sio Bwana Yesu! Ni mambo ambayo unatakiwa kufikiri, unataka kuolewa na nani.
Labda hujawahi kufikiria kitu cha namna hiyo, nataka nikufikirishe vitu vya kawaida kabisa. Wengine wanasema mimi nataka kuolewa na mtumishi, hesabu gharama kwanza! Wengine wanaona tunavyoshirikiana na mke wangu katika huduma  wanamtazama wanasema, wanataka kuolewa na mtumishi; kaamuulize mke wangu, tulipokutana hata wito haukuweko, na tulikutana wote hatujaokoka. Tulikuja kuokoka baada ya kuoana!
Mungu ametuteremshia utumishi tuko kwenye ndoa tayari, kwa hiyo usitamani ndoa ya kwetu, tamani ya kwako ambayo Mungu amekupangia. Mke wangu hakunipendea utumishi, sikuwa na tone la utumishi, wala hata ya kufanania ya kwamba nitaokoka, na yeye  alikuwa hajaokoka pia wakati huo. Lakini kwa saa na kwa makusudi na kwa utaratibu wa Mungu, tumekuwa jinsi tulivyo. Akatuteremshia utumishi wakati tumekwishaokoka na tumekwishaoana!
 Usijaribu kufananisha ndoa yako na ndoa ya mtu mwingine, hujui iliko toka, tamani ya kwako. Sasa unasema wewe unataka mtumishi, lakini watumishi wako wengi sana, kwa hiyo unataka mtumishi wa namna gani? Lazima ufikiri juu ya hili pia. Unasema mimi ninataka mhubiri, hata nabii ni mhubiri, mwinjilisti ni muhubiri, mwalimu anaweza akahubiri. Kitabia hawafanani, haleluya! Nataka nikufikirishe ikusaidie, maana nataka nikujengee msingi mzuri wa maisha ambao ukikanyaga vizuri shetani alie tu, maana hatawezi kukuvuruga.
Maana watu wengi wanapata shida sana wanapotaka kuoa au kuolewa, utakuta wanasema, mimi ninataka kuoa au kuolewa na  mtumishi, hayo ni maombi ya mtu ambaye hajaenda shule ya Roho Mtakatitu, bado yuko chekechea, unajua lazima uwe ‘very specific’. Mungu anataka useme naye kile kitu unachokisikia ndani yako. Anajua kabisa kitu ambacho ni kizuri kwa ajili yako; lakini Mungu hataki kukulazimishia tu, anataka ushirikiane naye, ili akikupa kitu ukipokee kwa furaha.
Kwa hiyo kama unataka mtumishi, ni muhimu useme unataka mtumishi wa aina gani. Kwa mfano ukisema nataka mwinjilisti, hesabu gharama, lazima uwe na neema ya kukaa na mwinjilisti. Si unajua mwinjilisti hakai nyumbani, anazunguka, akikosa watu wa kuwachapa injili huko nje, anakuja kuchapa injili nyumbani hata kama mmeokoka wote! Na ujue hawezi kumaliza ibada ya jioni mpaka awepo mtu wa kutubu, hajatubu ataendelea kufanya maombi.  Kama hauko tayari kuchukuliana  na mtu wa namna hiyo usiamue kuoa au kuolewa naye.
Lazima useme; au kama unataka kuolewa na nabii jipange, kwa sababu hajui kuongea na watu, muda wake mwingi yuko kimya, manabii mara nyingi wanafungwa midomo sio wasemaji ni mtu mkimya. Mara nyingi amejifungia kuomba peke yake na Mungu.  Hata saa nyingine unatamani uombe pamoja naye, lakini  Mungu anataka yeye peke yake. Wewe nenda kwenye biblia utaona maisha yake yalivyo kila kitu kinachomzunguka, kila kitu anachovaa, kila kitu anachokutana nacho, Mungu anaweza akakigeuza ujumbe.
Kwa hiyo usije ukashangaa kesho akakutazama na akaishia  kupata mahubiri toka kwako, halafu mkirudi nyumbani mnaanza kugombana, na unamuuliza sasa  wewe ulikuwa unanihubirije? Kwani wewe hukujua ya kwamba ni nabii na anaweza kupata ujumbe unaosema: “kama vile mke wako alivyovaa, ndivyo na kanisa langu lilivyo asema, Bwana”!
 Wewe usifanye mchezo! Sasa nyingine mnaishiwa chakula na anaona jinsi mnavyohangaika, basi utakuta amekwishapata ujumbe kama huu, “kama vile mke wako alivyokuwa anahangaika kutafuta chakula kwa ajili ya watoto, ndivyo na mimi ninavyotafuta chakula kwa ajili ya watoto wangu, asema Bwana”!
Saa nyingine unavaa nguo zinapasuliwa, mpaka viungo vya ndani vinaonekana, ujumbe unatoka saa hiyo mara moja, anasema, “Kama vile mke wako alivyovaa nguo iliyopasuliwa na watu wanaona ndani, ndivyo na kanisa langu lilivyo vazi lake limepasuliwa na shetani anaona ndani”!
 Lazima uwe tayari kuwa ujumbe, kama unataka kuolewa na nabii. Uwe tayari kuwa ujumbe, hujawa tayari usiombe uolewe na nabii! Unataka kuolewa na mchungaji uwe na moyo mkubwa wa kupokea wageni. Mwingine anasema mimi ninataka kuolewa na mtumishi lakini ndani yake anawaza mtu anayezunguka na kuhubiri, kumbe Mungu ameweka ndani yake mtumishi, lakini ni mfanya biashara.
Mfanya biashara mwingine anapakwa mafuta kufanya biashara, ndio sehemu yake kumtumikia Mungu, mwingine ni fundi cherehani, mwingine ni dereva, wanapakwa mafuta sehemu zao hizo za utumishi, usije ukafikiri hao wanaoafanya kazi nyingine sio watumishi wa Mungu. Mungu anawapaka mafuta kwa ajili ya hizo kazi, ili walitumikie kusudi lake.
 Kwa hiyo unapokwenda katika maombi unasema tu mimi ninaomba mtumishi, Mungu atakuletea mtumishi yoyote, wako wengi, wengine wanafagia barabara, ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha kule kwenye vyoo vya kulipia ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha nyumba za watu, nao ni watumishi wa Mungu,oh haleluya!
 Mungu akikuletea mtumishi yeyote unaishia kusema, mimi sikuomba huyu niliomba mtumishi. Mungu atakuambia huyu ni mtumishi wangu, usimnenee kitu cha namna hiyo.
Kama msichana ni mfupi usitamani kijana mrefu, au kijana ni mrefu unatamani msichana mfupi. Kwa kweli, sio kwamba Mungu hawezi kukupa, lakini wewe fikiri tu mwenyewe, haleluya! Maana mwingine anakuwa mfupi kiasi ambacho anafanana kama vile ni mtoto kwako, wenzako wanakuuliza tangu lini umepata mtoto na akakua na  akawa mkubwa namna hii, unasema “ninyi msiseme hivyo, ni mume wangu huyu”.
 Ni uamuzi wako. Sasa, si lazima mfanane urefu, lakini msipishane sana; kwa kweli ni kwa faida yenu wenyewe, haleluya!
Kama msichana hupendi mwanaume mwenye ndevu, omba vizuri. Maana unaweza ukapata mtumishi wa Mungu, lakini ana ndevu na wewe huzitaki. Ikifika siku umeingia tu kwenye ndoa kitu cha kwanza unamtafutia wembe ili anyoe ndevu zake – hii ni kumwonea! Ulimpenda akiwa na ndevu, kumbe wewe ulikuwa unamtegea tu ili baada ya arusi tu umpe wembe! Wako wasichana wanaopenda wanaume wenye ndevu, waachie hao!
Huyu Bwana Mungu wetu ni mzuri sana, unajua, saa nyingine huwa ninawaza jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na nabaki ninashangaa sana. Maana kuna wanaume wengine hata ndevu hawana, hata wakilazimishia kunyoa kidevu kitupu  haziji. Sasa mtu mwingine anajisikia vibaya, akifikiri ya kuwa mtu anaonekana ya kwamba yeye ni mwanaume kwa sababu tu ana ndevu, si kweli. Kuna wanaume wengine wametengenezwa namna hiyo ‘special’ kwa ajili ya wasichana wasiotaka wanaume wenye ndevu, haleluya!
  Maana mwingine anaweza akaachia ndevu zikafunika mpaka karibu na kwenye pua. Sasa kama ni mtu  mweusi sana  ‘ni hatari sana’, giza likiingia tu ndani ya nyumba wewe unamwambia ‘cheka’, akicheka yale meno yake yanaweza yakamulika kidogo, na utajua yuko wapi! Hivi vitu ukishaingia kwenye  ndoa ni vitu vikubwa sana, kuliko watu wanapoviangalia kabla hawajaoana.
Wewe unakuta kijana anaoa msichana ana rangi nyeusi nzuri tu, akifika ndani unamletea madawa ajikoboe, wewe ulikuwa unamwoa wa nini? Hiyo sasa ni sawa na kumwambia Mungu kwa kweli nimechukua tu huyu, lakini sio niliyekuwa namtaka!
 Niliyekuwa namtaka ni mweupe, sasa maandamu umenipa huyu wacha nimkoboe mpaka afike rangi ninayotaka, - haviendi namna  hiyo bwana! Mungu alipokuwa anamuumba huyo msichana namna hiyo aliona, alimtazama alivyo na weusi wake huo akaona kila kitu chema, akajipa sifa, akajipa maksi asilimia mia moja, amefanya kitu chema!
 Sasa akitaka kupaka rangi  hiyo ‘nyumba yake’ na kuinakshi ni kitu kingine. Unajua kuna nyumba nyingine hazipendezi mpaka uzipake rangi fulani, haleluya! Mwili ni nyumba, kuna wengine hawawezi kupendeza mpaka wamepaka rangi fulani kwenye miili yao. Sasa utapata mtihani mgumu, nimeona, kijana anampenda msichana, lakini msichana anaweka rangi kwenye midomo yake, kucha zake anaweka rangi, anachora na kalamu hapa kwenye nyusi kidogo, ukimtazama vizuri usoni utagundua ya kwamba ameweka kitu kingine juu ya uso wake.
 Umempenda akiwa namna hiyo. Wakati ulipokuwa unamfuatilia hukumuuliza hayo maswali, leo ameingia ndani umemuoa, unamwambia sitaki hizo rangi! Hiyo ni kumwonea,  maana ulimkuta akiwa hivyo, kama ulikuwa humtaki akiwa amejinakshi na rangi hizo, hukutakiwa kumfuatilia, wako wengine ambao watakuwa radhi na huyo anayejipaka rangi!
Kuna kijana alioa msichana, wamefika ndani wakaanza kugombana naye habari za nywele, mpaka akamrudisha kwao, - nywele tu! Huyu dada kaenda katengeneza nywele staili fulani, yule kijana haitaki. Lakini alimkuta yule msichana anatengeneza nywele kwa staili hiyo, sasa kwa nini hivi vitu hawakutaka kuzungumza kabla ya kuamua kuoana?
 Mimi ninataka nikusaidie upunguze ugomvi ndani ya ndoa utakayokuwa nayo; maana vitu ambavyo Mungu atawaletea vya kufanya pamoja kwenye ndoa ni vikubwa kuliko mnavyofikiri, kiasi ambacho hamhitaji kutumia muda wenu kushindania vitu vidogo vidogo ambavyo mlikuwa muwe mmekwisha kuvijadili kabla ya kuoana. Mna mambo muhimu sana ya kufanya, kiasi ambacho kuanza kushindana na kubishana juu ya  vitu ambavyo mlitakiwa muwe mumeshavizungumza kabla ya kuoana; huko ni kutokuelewa utaratibu wa Mungu ulivyo juu ya kumpata mwenzi wa maisha
9:UKO TAYARI KUOLEWA LINI,MAANA YAKE MUDA GANI AMBAO UNGETAKA KUOA AU KUOLEWA.


Utasikia mwingine anasema, siku Mungu atakapo nipa mume au mke, hii ni hatari sana! Biblia inasema kwenye kile kitabu cha Mhubiri.3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”.
 Kila kitu kilichoko chini ya mbingu kimeratibiwa, kwa lugha nyingine, ni kwamba  kila mwanadamu ana kalenda yake, iko kalenda yako ya kuzaliwa, na ipo kalenda ya  matukio na mipango mbalimbali. Mungu anaijua. Mungu anatangaza mwisho tangu mwanzo, anajua mwisho wa maisha yako wakati wewe unapozaliwa.
 Katika mwanzo wa maisha yako, Mungu anakuwa amekwishajua mwisho wako; utakavyokuwa; na kama amekwishajua mwisho wako, maana yake ameshatembea kwenye maisha yako yote toka mwanzo mpaka alipofika mwisho, na alipokamilisha maisha yako akarudi mwanzo ndipo akakuongoza kuzaliwa.
Mungu anapokuacha uzaliwe duniani, hakika ujue kabisa ya kwamba amekwisha tembea na wewe katika maisha yako, amesharatibu mambo yako na yako hatua kwa hatua; kwa mfano, kitu gani utafanya, wapi utasoma, utasoma nini, utaolewa na nani au utaoa nani na itakuwa, lini, maisha yako yatakuwaje, utamtumikiaje, mpaka mwisho wako.  Akiishafika mwisho wa maisha yako anarudi mwanzo, akishafika mwanzo anatangaza mwisho tangu mwanzo; kwa hiyo kuanzia hapo unapozaliwa ujue maisha yako yote yamesharatibiwa!
Ni vizuri ufahamu hii mistari itakusaidia, maana inakujengea msingi mzuri wa maisha hapa. Isaya.46:9-10 inasema, “Kumbukeni mambo ya zamani za kale maana mimi ni Mungu wala hapana mwingine, mimi ni Mungu wala hapana aliye kama mimi. Nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado, nikisema, shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote”.
Kwa lugha nyingine anatuambia ya kwamba, ‘wewe unaona kila kitu ni kipya, unapoishi kila siku ni mpya, kila dakika inayokuja ni mpya, Mungu anasema hiyo safari unayopita, mimi nilikwishaipita tayari, nikafika mwisho wa maisha yako ndipo nikakuruhusu uzaliwe. Ulipokuwa unazaliwa nikatangaza mwisho wako tangu wakati unazaliwa.
 Sasa mimi ninataka nikuambie kama Mungu anajua, na shauri lake anasema litasimama katika maisha yako, ili mapenzi yake ayatende katika maisha yako, unahitaji kuwa mwangalifu. Kwa sababu kuna mpango na saa ya Mungu ya kuoa au kuolewa, -  ipo!
Mungu anapokuletea mawazo ya kuoa au kuolewa, ni kwa ajili yakuimarisha maisha yako na wito wako na kazi na makusudi, ambayo ameyaweka hapa duniani. Atakuletea mtu atakaye imarisha wito wako, atakuletea mtu atakaye saidiana na wewe, uwe ni mwanamke au uwe ni mwanaume.
Mungu anapo kukutanisha na mtu wa kuoana naye ni kwa ajili ya kuimarisha nguvu zenu ili mtimize kusudi la Mungu. Kwa hiyo lazima anajua kuna saa huyu mvulana anahitaji mke, au huyu msichana anahitaji mume! Lakini watu wengi sana hawalifuatilii hili. Wakati sisi tunaoana na mke wangu tulikuwa bado vijana, tulioana hatujafikisha hata miaka thelathini, ninakumbuka nilikuwa na miaka 28. Tulijaliwa kuwapata watoto tungali bado vijana sana. Lakini tuna watoto ambao ni  wakubwa kwa sasa. Tumefika kipindi ambacho tunaweza tukafuatilia masuala ya utumishi kwa namna ambayo haiwaumizi watoto wetu sana!
Maana watoto wakiwa wadogo wote, mimi ninakuambia kumtumikia Mungu ni kunakuwa kugumu sana, usije ukafikiri ni kurahisi. Maana unahitaji kuwa karibu nao; wanahitaji kusoma shule, wanahitaji kufanya vitu mbalimbali, wanahitaji kuwa na baba karibu, wanahitaji kuwa na mama karibu. Saa nyingine mnataka kusafiri nao; unaweza ukasafiri nao lakini usije ukafikiri ni kitu kirahisi.
 Tulisafiri na Joshua (mtoto wetu wa nne) akiwa na wiki sita. Sijawahi kuona watu wakisafiri na watoto wao wakiwa wadogo namna hiyo, Joshua alikwenda kwenye huduma akiwa na wiki sita tu. Hatukuwa na namna ambavyo tungeweza kumwacha. Sasa unaweza ukaelewa akiwa na wiki sita; maana yake mama yake ana muda wa wiki sita tu tangu ajifungue na tulisafiri kwa gari, sio kwa ndege, bali kwa gari!
 Tulisafiri masaa karibu kumi na mbili, tumebeba kila kitu, tumebeba mpaka unga wa kutengenezea uji, na beseni la kuogea, na maji. Huwezi kumwogeshea mtoto mchanga wa wiki sita maji yoyote tu, kwa hiyo tulibeba maji ya kumwogeshea. Huwezi kwenda ‘spidi’ unayotaka, ikifika saa yake ya kula lazima usimame! Ukifika kwenye hoteli huwezi kumlaza jinsi unavyotaka, lazima uingie kwanza uombe, uangalie yale  mashuka yaliyoko halafu uombe, uangalie kile kitanda halafu uombe, uangalie kila kitu kule ndani halafu uombe!
 Wewe ni mtumishi wa Mungu, ukienda na mtoto kienyeji kienyeji tu, ibilisi anaweza akamvamia na ukapata shida, na huduma yako yote uliyoiendea ikaharibika. Unaweza ukatamani saa nyingine usinge- safiri naye. Lakini mnaposafiri pamoja, kumbuka ina gharama yake.
Lakini mambo haya  unahitaji kufiri mapema, ili uweke kwenye agenda yako ya maombi ujue kabisa mpango wa Mungu ya kuwa unatakiwa kuoa au kuolewa lini. Ninajua kwa wengi kinakuwa kigumu hicho, maana wengine wametamani kuolewa jana, hawajapata wanaume, wengine wangetaka kuoa leo, lakini bado hawajapata msichana wa kuoa.
Wengine wanatamani kuolewa si kwa sababu mpango wa Mungu umefika wa kuolewa; ila ni kwa sababu wanaona muda wao wa kuolewa umefika, wengine wanaona umri umesogea. Mpango wa Mungu juu ya maisha yako, haubabaishwi na jinsi wewe unavyohesabu miaka,jirani zako wanavyohesabu miaka, ndugu zako wanavyohesabu miaka, au rafiki zako wanavyohesabu miaka.
 Mungu anajua alichopanga kwa ajili yako, ana kalenda yako kabisa, na kila alichokichagua Mungu ndicho sahihi.
10:UKO TAYARI KUZAA,KUTUNZA NA KULEA WATOTO WANGAPI?

       Niliuliza vijana fulani ambao ndio wametoka tu kuoana, wanafurahia maisha yao, ghafla  nikawauliza swali ambalo hawakutegemea, nikawauliza, “mna mpango wa nakuzaa watoto wangapi? Walinitazama wakasema, “Mungu anajua”. Nikawambia; “siyo hivyo! Mungu anajua lakini ninyi je?” “Wakasema hatujui”, nikawaambia hayo ndio makosa ya wengi waliomo katika ndoa.
Sasa ninakueleza hivi kwa sababu ni vitu ambavyo Mungu alisema na sisi  mapema. Hakuna mtoto aliyezaliwa baada ya sisi kuokoka ambaye sikujua ya kwamba atazaliwa, na hakuna mtoto aliyezaliwa baada ya sisi kukuokoka ambaye sijajua wito wake. Na Mungu aliponyamaza na hakutuonyesha mtoto mwingine, hatukuona sababu ya sisi kutafuta  mtoto mwingine. Wengine wanafikiri Mungu hana mipango ya uzazi (kasome biblia yako vizuri) – Mungu ana utaratibu wa uzazi kwa kila ndoa anayoisimika.
Ni kitu ambacho unahitaji kuomba, ili Mungu akujulishe. Nimeona watu wakishindana ndani ya ndoa, baba anataka watoto wengi, mama hataki. Nimekuta ndoa nyingine mama anataka watoto wengi wamzunguke kama timu ya mpira lakini baba  hataki. Na ugomvi mkali unatokea juu ya hili.
Mwingine anamzalisha mke wake kila mwaka (unaelewa maana ya kila mwaka?) si unaelewa mimba inakaa miezi tisa tumboni, kwa hiyo anaweza akazaa kila mwaka! Sasa umewahi kufikiri kila mwaka unazaa, kwa hiyo ikiwa uko kwenye ndoa miaka kumi basi una watoto kumi. Au mtu yuko kwenye ndoa miaka mitano, tayari ana watoto wanne na bado anaendelea kuzaa – hii ni sawa?
Nilikwenda mahali fulani kwa ajili ya huduma dada mmoja alikuwa anafurahia muujiza wake wa tumbo, jinsi ambavyo Mungu amemponya, akasema, “sasa nitakuwa tayari kuzaa mtoto mwingine”. Nikamuuliza, “una watoto wangapi sasa?” Akasema, “wanne”. Nikamwambia, “Na bado unahitaji mtoto mwingine”. Akasema, “ndio, ninataka mtoto mwingine”! Unajua kwa nini ninakueleza vitu vya namna hii, - kwa sababu kila mtoto ana wajibu wake, ana mzigo wa kwake na anatunzwa kivyake!
Kadiri unavyozaa watoto wengi, ndivyo unavyozidi kuwa na wajibu mkubwa zaidi wa kulea. Watoto hawafanani, huwezi ukawalea kijumla. Watoto hawalelewi kwa namna hiyo. Kila mtoto ameitwa kivyake, ana mpango wake, ana njia yake, ana tabia yake na ana namna yake ya kutunzwa,– hawafanani!
Mtoto anayezaliwa lazima umlee kwa uangalifu. Hujamfikisha mahali katika kumlea, tayari ameshakuja mwingine, unafikiri mchezo!
Hao watoto wawili hujawafikisha mahali katika kuwalea tayari ameshakuja mwingine, ni kitu kigumu hujawahi kuona! Huyu wa kwanza hapati tena ule umuhimu wake na nafasi yake, kwa sababu sasa  anakimbiliwa huyu aliye mdogo; akija mwingine anakimbiliwa aliye mdogo zaidi,  hao waliotangulia wanajikuta wanakua kivyao.
Watu wengi wanabaki kushangaa kwa  nini watoto wengi waliozaliwa kwa kufuatana saa nyingine kwa karibu wanagombana. Ni kwa sababu huyu mkubwa anaona ameingiliwa na huyu mdogo, na huyu mdogo anaona kwamba huyu mkubwa ameshakuwa mkubwa, kwa hiyo mimi niliye mdogo ndiye mwenye haki zaidi. Ni ugomvi unaoweza ukaendelea mpaka wamekuwa watu wazima.
 Mimi nimesoma masuala ya uchumi, sijasomea masuala ya kuhubiri. Si kwa sababu sikupenda kusomea kuhubiri, lakini hakuwa mpango wa Mungu wa kunilea namna hiyo katika wito. Kuna wengine Mungu anawapanga na kulea wito wao kwenye vyuo vya biblia; na ni mpango wa Mungu tu mzuri. Lakini Mungu alikuwa na mpango mwingine na mimi. Mimi katika chuo  nilikwenda kusoma masuala ya uchumi.
Sasa, siku moja nchi hii ilitembelewa na wageni, wa kutoka Washington D.C, wa shirika la fedha ulimwenguni. Wale watu wakatuuliza maswali, hebu tuambieni mabadiliko ya uchumi yanayoendelea hapa nchini ninyi mnayaonaje.
Mama mmoja akanyoosha mkono, akasema, “Tunaelewa umuhimu wa mabadiliko mengine yanapotokea katika uchumi wa nchi, kwa sababu ya mazingira tunayoyaona hasa tunapoona vitu vingine havifanyi kazi. Kwa hiyo kuna umuhimu wa kubadilisha sera zingine ili mambo yaende sawasawa.
Lakini tatizo tulilonalo, ni kwamba maandalizi ya kutuandaa sisi kama watanzania ya kwamba kuna mabadiliko yanakuja, hayo maandalizi hayajafanyika ya kutosha”. Wakasema, “mama tupe mfano”. Akasema “kwa mfano, tunatakiwa kuchangia masuala ya afya, tunatakiwa kuchangia masuala ya elimu, kama tungejua kwa mfano, miaka mitano au sita kabla, kwamba miaka sita ijayo au miaka kumi ijayo, ya kuwa pamoja na kwamba sasa elimu ni bure, afya ni bure, iko siku mtahitaji kutoa pesa zenu mfukoni ili kulipia gharama hizi – tungekuwa waangalifu tunazaa watoto wangapi.”
 Nikagundua mara moja kwamba huyu mtu wazo lake lilikuwa ni zuri kabisa.Kwa sababu kwa watanzania wengi inapofika mtoto anazaliwa walijua anayewajibika kumpeleka huyo mtoto shule ni serikali, anayewajibika kumlipia gharama za hospitali ni serikali! Wewe utazaaje ili serikali ikutunzie mtoto? Lazima na wewe uwe na bajeti yako!
 Unajua biblia haisemi serikali leeni watoto,  inaasema enyi wakina baba leeni watoto. Soma Waefeso 6:4. Sasa pale serikali itakapokusaidia wacha ikusaidie, lakini usikae unajiambia ya kuwa mimi nimezaa watoto kumi na tatu, lazima waende shule bure, lazima waende kwenye hospitali bure. Nani anayegharamia hizo huduma, unafikiri ni za bure? Hakuna! Wewe unaona huduma hizo ni bure, lakini yuko mtu ametoa pesa  za kugharamia hizo huduma toka mahali fulani.
 Nakumbuka wakati fulani nlikuwa Zimbabwe, baba mmoja aliyekuwa na cheo kikubwa tu kwenye makanisa ya kule Zimbabwe, tulikuwa tunazungumza naye siku moja juu ya masuala ya kusomesha watoto. Alisema wakati mmoja alikwenda Ujerumani kwenda kutafuta watu wa kuwasomesha watoto wake.
Yule mzungu ambaye alikuwa anazungumza naye, akaamuuliza, “ndugu una watoto wangapi, akasema sita”. Akasema, “unajua mimi nina watoto wangapi.” Akasema, “sijui”. Akasema watoto wawili”. Akasema, “unajua ni kwa nini hatutaki kuzaa watoto wengi, usije ukafikiri tunachukia watoto, hasha ila ni  kwa sababu ya gharama, za kuwatunza zilivyo kubwa”.
 Tunataka angalao kila mtoto atunzwe vizuri na aende shule nzuri, wakiishakuwa wengi inakuwa si rahisi kuwagharamia wote ipasavyo, na  inabidi ugawe ulichonacho kidogo kidogo. Wanaishia wote shule ya msingi, kwa sababu huna hela ya kuwapeleka sekondari. Akasema, “sasa ninyi waafrika mambo yenu hayako sawa, wewe unaona mimi nimezaa kidogo nimejinyima kwa ajili ya watoto wangu wasome vizuri, sasa unataka fedha ya kwangu nikusomeshee watoto wa kwako ambao wewe umezaa bila kufikiria jambo la gharama ya kuwatunza wakiishazaliwa?”
 Aliambiwa kitu cha kweli usoni na mzungu! Unaweza ukafikiri alikuwa anamtukana, lakini alikuwa anamweleza kitu cha ukweli; watu wengi sana hawafikiri hiki kitu. Wale wazee wa zamani walikuwa wakizaa kwa mahesabu huku nyuma. Akizaa watoto wa kike wengi ana hesabu ng’ombe atakazopata watakapoolewa, usije ukafikiri ana hesabu gharama, bali ana hesabu ng’ombe atakazopata! Watoto wa kike kwake ni mradi. Akizaa watoto wa kiume anajua amepata nguvu kazi ya kulima mashamba, walikuwa wana mahesabu yao.
Lakini sasa hivi lazima ukae ufikiri kwa namna nyingine,sikuambii ya kwamba kuwa na watoto wengi ni kitu kibaya, ni uamuzi wako! Kama unataka kwenda na mstari unaohimiza mkaongezeke mkaijaze nchi (Mwanzo 1:28) hakuna shida! Unaweza ukaendelea na wewe ukawa kwenye kuijaza nchi, lakini usikazane kuijaza nchi halafu unataka wengine wakusaidie kulea watoto hao -  hiyo sasa sio sawa!
 Mimi sijui kwa upande wako, na sijui kwa upande wa wazazi wako, lakini ninakueleza ili baadaye uwe mzazi mzuri, ni vitu unahitaji kufikiri mapema. Niliwaambia watoto wangu siku moja, nikawaambia sikiliza, tumejiwekea maamuzi ndani ya hii  nyumba mimi na mama yenu, ya kwamba ni wajibu wetu kuwasomesha mpaka chuo kikuu ili angalau kila mmoja awe na shahada ya kwanza, huo ni wajibu wetu.
 Baada ya shahada ya kwanza ukitaka kuendelea Mungu akubariki. Mungu akitupa nafasi ya kukusaidia kuendelea zaidi ya shahada ya kwanza tutakusaidia. Lakini tumemwomba Mungu atusaidie, kila mtu lazima afike chuo kikuu. Unajua kama usipoweka malengo ya namna hii, hata matumizi yako na bajeti yako haviwezi kukaa sawa. Ndio maana ninakuambia lazima umwombe Mungu akusaidie, usije ukafikiri kusomesha watoto ni kitu rahisi.
Ninyi mnajua ambao mko shule, wengine wameshindwa kuendelea na shule kwa sababu wazazi wameshindwa kutoa karo za shule, na sio kwa sababu wanafunzi hawataki kuendelea na shule, lakini ni kwa sababu hakuna fedha za kuwasomesha.
Nilimuuliza msichana mmoja katika mkoa mmoja wakati nilipokuwa huko kwa huduma, nikamuuliza “umemaliza darasa la ngapi”. Akasema, “kidato cha sita”. Nikamwambia, “sasa kwa nini hutaki kuendelea na shule?” Akanitazama usoni, halafu akasema, “sithubutu hata kumwambia baba anisomeshe zaidi maana  ninawaangalia wadogo zangu huku nyuma walivyo na ninaangalia na hali ya baba yangu aliyonayo kifedha, amenisaidia nimefika kidato cha sita, sasa nikifikiria wadogo zangu – ambao bado wako shule za msingi, naona wacha na wao basi wasogee sogee angalau wafike sekondari na wao kama mimi. Kwa hiyo mimi nimenyamaza kimya”.
Huyu msichana amemaliza kidato cha sita  anataka kuendelea na masomo, lakini hawezi kuendelea kusoma kwa sababu anaangalia hali ya wazazi wake ilivyo, anajua kabisa angalau na wadogo zake na wao wasome, lakini sio kwamba anataka kuishia kidato cha sita
11:UKO TAYARI KUISHI KATIKA HIYO NDOA KWA MUDA GANI?

          Sasa ninakupa siri hapa ikusaidie, Kama umekaribia – karibia kuoa au kuolewa, na hujawahi kujiuliza maswali ya namna hii, basi Mungu anakuweka mahali pazuri kwa kukupa nafasi ya kusoma kitabu hiki. Labda nikuambie kitu cha namna hii kitakusaidia, kabla sijakupa mistari mingine kwenye biblia, ni hivi: Hakuna sababu ya kuolewa na kijana ambaye atakufa baada mwezi mmoja. Au hakuna sababu ya kuoa msichana atakayekufa muda si mrefu baada ya arusi yenu.
 Kwa nini uolewe leo uwe mjane baada ya miezi miwili? Na ukiishaolewa umekwisha badilisha kabisa hali yako na ya  mume wako; akiisha kufa wewe sio msichana tena, utaitwa mjane, hata kama umri wako ni mdogo. Tulienda mahali ulani tukasema tunaomba wajane tuwaombee, tulishangaa kuona ya kuwa robo tatu yao walikuwa ni wasichana. Ungeambiwa wameolewa ungekataa, lakini wamefiwa bado wana umri mdogo.
 Sasa mimi ninataka nikuulize swali, kwa nini unataka uolewe, halafu mume wako afe baada ya miezi miwili au unataka uoe mke wako afe baada ya mwezi mmoja, au baada ya mwaka? Hakuna kitu kinachosumbua kama hiki. Ngoja nikueleze hili tena ya kuwa ndoa ya pili sio ndoa ya kwanza. Ndoa ya kwanza ina utofauti wake, na ndoa ya pili ina utofauti wake.
Ikiwa unataka kuishi muda mrefu na mwenzi wako wa ndoa unahitaji;
1.     Kuwa mwangalifu kutii ile mistari ilioko kwenye biblia inayozungumzia juu ya muda wa mtu kuishi. Kwa mfano: Waefeso 6:1-3 inasema; “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, upate heri, ukae siku nyingi katika dunia”.
Kwa hiyo angalia uhusiano wako na wazazi wako kama bado wako hai. Lakini pia chunguza uhusiano wa huyo anayetaka kukuoa au anayetaka umuoe, na wazazi wake, kama bado wako hai.
2.      Omba Mungu akupe maisha marefu na huyo mwenzako hata kabla hamjaamua kuoana. Ili kama kuna mmoja wenu hataishi muda mrefu – basi Mungu awaarifu na kuwaongoza cha kufanya.
Mwingine anataka aingie kwenye ndoa kwa kubahatisha au kwa majaribio. Maana yake ndani ya nafsi yake anajiweka tayari kuachana na mwenzi wake kama anaona mambo ya ndoa yake hayaendi alivyotarajia. Mtu wa namna hii hataweza kuwa mvumilivu na mwepesi wa kutafuta suluhisho kukitokea tatizo katika ndoa yake.
Uamuzi wa kuoa au kuolewa unamtaka mtu aingie katika ndoa asilimia mia moja. Ikiwa hautakuwa tayari kuingia kwenye ndoa kwa asilimia mia moja – tafadhali usiamue kuoa au kuolewa. Utampotezea tu mwenzako – maana hakuna ndoa isio na matatizo. Lakini pia hakuna tatizo ambalo Mungu hawezi kulitatua. Lakini, je, uko tayari kushirikiana na Mungu katika ndoa kwa kiwango cha asilimia ngapi?.